Waziri Silaa atoa siku 30 kwa wadaiwa Kodi ya Pango la Ardhi

DAR-Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ametoa siku 30 kwa wamiliki wote wa ardhi wanaodaiwa Kodi ya Pango la Ardhi ambao hawajalipa hadi sasa kulipa kodi husika na baada ya muda huo kupita hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa.

Waziri Silaa ameyasema hayo Mei 10,2024 katika Ofisi za Wizara ya Ardhi zilizopo Magogoni jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa, kila mmiliki wa ardhi analo jukumu la kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka amepewa sharti la kulipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa kila mwaka kwa mujibu wa Fungu la 33 (1) la Sheria ya Ardhi (Sura ya 113).

Aidha, ameongeza kuwa kwa mujibu wa Fungu la 44 (1) la Sheria ya Ardhi (Sura ya 113), kila mmiliki wa ardhi anatakiwa kutimiza masharti ya umiliki ikiwa ni pamoja na sharti la kulipa Kodi ya Pango la Ardhi.

Silaa amesema, kitendo cha kutolipa Kodi ya Pango la Ardhi ndani ya muda uliowekwa na sheria, kinasababisha mmiliki wa ardhi kuvunja moja ya sharti la umiliki.

Ameongeza kuwa, wizara kwa nyakati tofauti, imekuwa ikihamasisha na kuwakumbusha wamiliki wa ardhi kulipa Kodi ya Pago la Ardhi. Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa ardhi hawajatekeleza wajibu huo wa kisheria.

“Naelekeza wamiliki wote wa ardhi wanaodaiwa Kodi ya Pango la Ardhi, kulipa kodi husika ndani ya siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya tangazo hili. Baada ya muda huo kupita, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na wamiliki hao watafikishwa mbele ya Mahakama na taratibu za kisheria za ubatilisho wa milki zao zitaendelea,”amesema Silaa.

Silaa amehitimisha kwa kusema kuwa katika kipindi hicho cha siku 30, vituo vya makusanyo ambavyo ni; Ofisi za Ardhi za Mikoa na Ofisi za Ardhi za Halmashauri zote nchini, kwa siku za kazi zitakuwa wazi hadi muda wa saa 2:00 usiku.

Hivyo, naagiza watendaji wote wa Sekta ya Ardhi, kuratibu mazingira rafiki kwa ajili yakufanikisha utekelezaji wa mkakati huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news