Azam FC yaichapa Singida Black Stars mabao 2-1

DAR-Azam FC imechukua alama zote tatu dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ni kupitia mtanange ambao umepigwa Novemba 28,2024 katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 38 ndiye aliyeanza kufungua pazia la magoli ambapo bao lake lilidumu hadi kipindi cha mapumziko.

Bao hilo lilipatikana baada ya kumalizia pasi safi kutoka kwa Idd Seleman (Nado) ikiwa ni bao la tatu kwa Feisal Salum katika msimu huu.

Katika kipindi cha pili,Jhonier Blanco alipachika bao la pili dakika ya 57 ambalo lilionekana kuwatia hasira Singida Black Stars.

Elvis Rupia aliwaoatia Singida Black Stars bao la kufutia machozi dakika ya 62 baada ya kumalizia krosi ya kiungo Josaphat Arthur Bada.

Pengine haya si matokeo ya kuvutia sana kwa kocha Msaidizi Ramadhan Nswanzurimo ambaye aliteuliwa Novemba 25, 2024 kuchukua nafasi ya Patrick Aussems aliyesimamishwa kazi pamoja na msaidizi wake Denis Kitambi ndani ya Singida Black Stars.

Matokeo yasiyoridhisha ya Singida Black Stars ndiyo yalisababisha wawili hao kufutwa kazi.

Kwa matokeo Azam FC wamekwea mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara wakifikisha alama 27.

Ni baada ya mechi 12 huku Singida Black Stars wakisalia nafasi ya nne kwa alama 24 baada ya mechi 12.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news