NA DIRAMAKINI
RATIBA ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Novemba 28,2024 inatarajiwa kuendelea kwa mchezo mmoja kati ya Azam FC dhidi ya Singida Black Stars.
Mtanange huo utapigwa leo katika Dimba la Azam Complex uliopo Kata ya Chamanzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Leo mtanange huo ni muhimu kwa timu zote ikizingatiwa kuwa, Azam FC ambayo ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ina alama 24 baada ya michezo 11 ya awali.
Aidha, Singida Black Stars nayo ina alama 24 baada ya michezo 11 ambapo ipo nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara huku wakitofautiana kwa magoli.
Katika ligi hiyo ambayo ina timu 16, Simba Sports Club wapo kileleni kwa alama 28 na watani zao Young Africans Sports Club (Yanga SC) ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 24 zote baada ya michezo 11.
Aidha,Kengold FC inaburuza mkia katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania kwa alama sita baada ya michezo 12 huku ikifuatiwa na Pamba Jiji FC yenye alama nane baada ya mechi 12.
Wakati huo huo,Singida Black Stars inashuka dimbani leo bila makocha wake Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi ambao walisimamishwa kazi hivi karibuni.
Uamuzi huo ulitokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika mechi zake tatu zilizopita za NBC Premier League.
Katika mechi 11 za NBC Premier League, ambazo Singida BS ilishacheza, imeshinda michezo saba, imetoka sare mechi tatu na kupoteza mchezo mmoja ambao ni dhidi ya Yanga SC.
Aidha,kwenye kipindi hiki ambacho makocha hao hawatokuwa kazini, kikosi cha Singida BS kitaongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Ramadhan Nsanzurwimo akisaidiwa na Muhibu Kanu.
Nini kitatokea mchezo kati ya Azam FC na Singida Black Stars leo? Tusubiri dakika 90 zitaamua pale Chamanzi Complex.