NA DIRAMAKINI
TANZANIA imeendelea kuchanja mbuga katika soka baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuipandisha kwa nafasi sita kwa ubora duniani.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya viwango vya ubora wa soka duniani kwa mwezi Novemba,2024 ambapo FIFA imeipandisha Tanzania kutoka nafasi ya 112 na sasa inashika nafasi ya 106.
Kenya imeshuka kwa nafasi mbili kutoka 106 mpaka 108 huku Uganda wakiporomoka kwa nafasi moja.
Ni kutoka nafasi ya 87 mpaka nafasi ya 88 wakati Zambia wakipanda kwa nafasi saba kutoka nafasi ya 94 mpaka 87.
Rwanda katika viwango hivyo ipo nafasi ya 128 huku Burundi ikishika nafasi ya 139.
Katika orodha hiyo, mataifa 10 bora kwa soka barani Afrika namba moja inashikiliwa na Morocco ambayo pia inashika nafasi ya 14 duniani.
Aidha, kwa mujibu wa FIFA nafasi ya pili kwa ubora barani Afrika inashikiliwa na Senegal ambayo kwa ubora duniani ipo nafasi ya 17.
Misri ipo nafasi ya tatu kwa mujibu wa FIFA huku kwa ubora duniani ikishika nafasi ya 33,Algeria wapo nafasi ya nne huku kwa ubora duniani ikishika nafasi ya 37.
Nafasi ya tano kwa ubora Afrika kwa mujibu wa FIFA inashikiliwa na Nigeria huku kwa nafasi ya 44 kwa ubora duniani.
Ivory Coast wapo nafasi ya sita barani Afrika huku kwa ubora duniani ikiwa nafasi ya 46, nafasi ya saba kwa Afrika inashikiliwa na Cameroon huku kwa dunia ikiwa nafasi ya 49.
Vilevile, Mali ipo nafasi ya nane kwa ubora barani Afrika na nafasi ya 51 duniani, Tunisia inashika nafasi ya tisa duniani huku kwa upande wa dunia ikiwa nafasi ya 52 na Afrika Kusini inashika nafasi ya 10 kwa Afrika na nafasi ya 57 duniani.
Wakati huo huo kwa upande wa mataifa 10 bora duniani kwa soka, nafasi ya kwanza inashikiliwa na Argentina, Ufaransa nafasi ya pili.
Uhispania ipo nafasi ya tatu, England nafasi ya nne, Brazil nafasi ya tano,Ureno nafasi ya sita,Uholanzi nafasi ya saba,Ubeligiji nafasi ya nane, Italia nafasi ya tisa na Ujerumani nafasi ya 10.