MORONI-Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu leo amekutana na mtangazaji mkongwe wa Sauti ya Ujerumani Bi.Ummulkheir Hamidou ambaye ni mtanzania mwenye asili ya Comoro.
Katika ziara yake ubalozini Bi Ummulkheir amepongeza juhudi zinazofanywa na Ubalozi huo kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Comoro hususan katika sekta za afya,elimu na biashara.Bi Ummulkheir ambaye anakumbukwa kwa sauti yake nzito redioni na kiswahili fasaha,ameridhia ombi la ubalozi la kushirikiana nae katika kukuza Kiswahili nchini Comoro na kueleza namna anavyoona umuhimu wa Kiswahili nchini Comoro.
Kwa upande wake Balozi Yakubu alieambatana na maafisa wa Ubalozi amemshukuru kwa kutembelea ubalozini hapo na kumshauri Bi Ummulkheir kuweka kumbukumbu za maisha yake katika kitabu iwe ni rekodi nzuri na mafunzo kwa vijana.Bi Ummulkheir amekuwa mtangazaji wa Sauti ya Ujerumani kuanzia mwaka 1979 hadi 2020 alipostaafu rasmi.Ametembelea Ubalozini leo akiambatana na mumewe Bwana Hamidou Ali.

