ZANZIBAR-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ,Mhe. Masoud Ali Mohammed, amesema Serikali, haitopenda kuona asasi za kiraia kubadilisha muelekeo na kujiingiza katika mambo yasiokuwa na faida kwa taifa.
Akizungumza na viongozi wa asasi za kiraia huko Tunguu, amesema serikali imekuwa ikizihitaji asasi hizo katika kuimarisha huduma za kijamii na maendeleo, hivyo sio vyema kuona zinakiuka malengo ya kuanzishwa kwake.Amezihakikishia asasi hizo kuwa Serikali itaendelea kuzilinda kwa kuzipa muongozo ili kuziepusha kujiingiza katika migogoro isiyo ya lazima ambayo haina faida kwa wananchi na taifa lao.
Naye Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali Zanzibar NGO'S, Ahmed Khalid Abdallah, amesema uwasilishaji wa taarifa za fedha na utendaji kazi wa Jumuiya hizo kwa kila mwaka ni jambo la kisheria.
Amesema, kuwasilishwa kwa taarifa hizo kunaiwezesha ofisi ya mrajis kuandika ripoti na kuiwasilisha Serikalini ili kutambulika jinsi ya utendaji kazi wa jumuiya hizo.







