DAR-Ushindi wa mabao 3-0 ambao Simba Sports Club imeupata dhidi ya Tanzania Prisons umewarejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Simba SC imemenyana na Tanzania Prisons leo Februari 11,2025 katika Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika mtanange huo, Simba SC walianza mchezo kwa kasi huku wakitafuta bao la mapema dakika 20 za mwanzo,wamefanya mashambulizi ya hatari sita langoni mwa Prisons, lakini kikwazo kikawa mlinda mlango Sebusebu Samson.
Jean Charles Ahoua aliwapatia bao la kwanza dakika ya 29 kwa shuti kali ndani ya 18 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe.Pia,Elie Mpanzu aliwapatia bao la pili dakika ya 45 kwa shuti kali la chini chini akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi ya Leonel Ateba.
Dakika moja baadae Ladaki Chasambi aliwapatia bao la tatu baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Kapombe.Matokeo haya yameifanya Simba SC kufikisha alama 47 baada ya kucheza michezo 18 na kurejea kileleni.

