DODOMA-Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amewasisitiza Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Bajeti wa Mikoa kuandaa Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2025/2026 wenye tija.
Ametoa msisitizo huo jijini Dodoma, wakati akihitimisha kikaokazi cha siku mbili cha Uchambuzi wa Bajeti na Mipango kwa Mwaka 2025/26.
Kikao hicho kiliwaleta pamoja wadau wa sekta husika ili kuainisha na kuibua maeneo ambayo mafungu yanaweza kushirikiana na kuleta ufanisi katika uandaaji na utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2025/26.Uchambuzi huo unalenga kuhakikisha uratibu wa shughuli za Serikali Kisekta unaboreshwa ili kuongeza ushirikiano na nguvu ya pamoja (Synergies) katika utekelezaji wa mipango kati ya Sekta zinazotegemeana.





