ARUSHA-Tuzo za TEHAMA 2025 zimeibua hamasa kubwa ya ushindani hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Priscilla Kessy akipokea tuzo yake ya “Mwanamke Mjasiriamali’ katika TEHAMA kutoka kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa wakati wa Tuzo za TEHAMA 2025 zilizofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
Mafanikio makubwa ya TEHAMA yaliyosherehekewa katika tuzo hizo yamekuwa chachu ya kuongeza ari ya ubunifu na ushindani.
Ukweli huo umo katika Kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga ambaye kabla ya utoaji wa tuzo hizo zilizokuwa katika kategori au vipengele mbalimbali, alisema:
"Leo hii (Ijumaa ya Februari 21, 2025) tupo katika kusherehekea mafanikio makubwa ya TEHAMA nchini," akiongeza kuwa tangu kuzinduliwa kwa Mkakati wa Uchumi wa Kidigitali mwaka jana, hatua kubwa zimepigwa na taasisi na watu mbalimbali katika kuimarisha sekta ya TEHAMA.
Katika tuzo hizo zilizoandaliwa na Serikali kupitia Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kushirikiana na wadau wake kama SoftVentures, Chama cha Watoa Huduma za Intaneti Tanzania (TISPA), makundi ya vijana kutoka vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini, walijitokeza kwa wingi kushuhudia Serikali ikiwatunuku washiriki wa Tuzo za TEHAMA 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga akieleza jambo kuhusiana na kuanzishwa kwa Tuzo za TEHAMA ambazo kuanzia sasa zitafanyika kila mwaka.
Mapokeo na hamasa yaliyoonekana ukumbini katika hoteli ya Nyota Tano ya Gran Melia, jijini Arusha vilimlazimu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa kutoa ahadi na maagizo, lengo likiwa ni kuiona sekta ya TEHAMA inakua kwa kasi nchini.
Akizindua na kutoa tuzo hizo za 2025, Waziri Silaa alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kila linalowezekana katika kuikuza sekta ya TEHAMA ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha nchi inakwenda kuujenga kwa kasi uchumi wa kidigitali.
Aidha, imeahidi kuwafikia Watanzania wote, lengo likiwa kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma katika sekta ya TEHAMA.
Alipongeza kuanzishwa kwa tuzo hizo, akisema zitasaidia kuchochea ubunifu wa masuala ya TEHAMA na kukuza sekta ya Tehama nchini ambayo ni muhimu katika uchumi wa kidijitali.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa akiwa na baadhi ya vijana wadau wa sekta ya TEHAMA kutoka vyuo vikuu nchini, wakati wa Tuzo za TEHAMA 2025 zilizofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
“Nioneshe furaha yangu kwa ubunifu huu kwa Tume ya TEHAMA na washirika wake kwa kuandaa tuzo hizi ambazo zinatambua mchango wa TEHAMA nchini.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mara zote amekuwa akitoa maelekezo ya kuhakikisha tunatekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa kitaifa wa miaka kumi (10), hivyo basi, tusingependa kumuacha nyuma hata mdau mmoja, lazima tushirikiane kuhakikisha sekta yetu ya Tehama tunaikuza.”
Aliiagiza Tume ya TEHAMA kuhakikisha Tuzo hizo zinakuwa endelevu na zinafanyika kila mwaka kwa weledi na viwango vya hali ya juu ili kuvutia wadau zaidi kushiriki.
“Naona hapa kuna vijana wengi wa vyuo vikuu. Hawa ndio wadau wakuu wa sekta hii, lazima wahamasishwe na kuwezeshwa kufikia malengo yao,” anasema Silaa.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga akiwa katika picha ya pamoja na washiriki kutoka Kampuni ya Mainstream Media Tanzania Limited ambao waling’ara katika Tuzo za TEHAMA mwaka huu zilizofanyika jijini Arusha hivi karibuni.
Alizitaka sekta binafsi na za umma kuwapa nafasi vijana hao kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye taasisi zao ili kukuza ujuzi kwa mambo ya Tehama wanayoyasoma vyuoni.
"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mara zote amekuwa akitoa maelekezo ya kuhakikisha tunatekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidigitali wa kitaifa wa miaka kumi (10), hivyo basi, tusingependa kumuacha nyuma hata mdau mmoja, lazima tushirikiane kuhakikisha sekta yetu ya Tehama tunaikuza.”
Akigusia kundi la pili ambalo Waziri Silaa alisema Dkt. Samia analipenda sana, kampuni changa za ubunifu, alisisitiza haja ya serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kuzikuza na ili ziwe na mchango mkubwa katika uchumi wa kidijitali.
Katika Tuzo hizo za kihistoria, washiriki 380 waliwasilisha kazi zao zilizochujwa kitaalamu na kuthibitishwa na Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte ambayo imekuwa na jukumu la kutoa ushauri na usimamizi katika mchakato wa tathmini ya tuzo.
Awali, akitambulisha tuzo hizo na kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema lengo la Tume yake kutoa tuzo hizo ni kuhamasisha watu kufanya ubunifu mzuri wa masuala ya TEHAMA nchini.
“Ni lazima kusherehekea na kutambua mchango wa kila mmoja kwa kuwa uchumi wa kidijitali hauwezi kujengwa na serikali pekee, bali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Ndiyo maana tukaona tuanzishe tuzo ambazo ziko katika makundi 22, tulihamasisha wabunifu kutoka kampuni, mashirika ya umma, na watu mbalimbali kushiriki tuzo hizi ambazo zimetuleta hapa leo,” alisema Dkt. Mwasaga na kuongeza kuwa, tuzo hizo ni jukwaa muhimu kwa viongozi wa sekta, watunga sera, na wabunifu kushirikiana, kuungana, na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini.
Alisema kutokana na umuhimu wa sekta ya TEHAMA sasa tuzo hizo zitakuwa za kila mwaka.
Tangazo la tuzo hizo kuwa za kila mwaka liliamsha shangwe miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, wengi wakieleza kuwa wamehamasika na wamepania kushiriki na kushinda katika tuzo za mwaka 2026.
"Binafsi nilichelewa kupata taarifa ila nina mambo mengi ya kuyaingiza kwenye Tuzo. Naamini ningeshinda tu, lakini si mbaya, mwaka kesho (2026) wengi unaotuona hapa tumepania kushiriki na kushinda,” alisema Omega Seyongwe, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Wengi wa wanafunzi hao walidai kuwa, wamehamasika, lakini walishindwa kushiriki kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja kuchelewa kupata taarifa katika vyuo vyao, lakini pia kubanwa na muda wa kufanya maandalizi ya Tuzo.
Baadhi ya washindi wa tuzo hizo akiwemo, Nafidh Ally Mola mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kozi ya Sayansi ya Kompyuta katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam na Dorice Malle kutoka Taasisi ya Mama Mia’s Soko walisema tuzo walizopata zimewajengea hamasa zaidi katika kazi zao za ubunifu kwa kuwa zimewapa heshima katika jamii.
Mola alikuwa kivutio kwani mara baada ya kupokea tuzo yake, alikuwa mwenye furaha isiyoelezeka bubujikwa na machozi kutoka jukwaani hadi sehemu aliyokuwa amekaa, akifanya hivyo kwa dakika kadhaa huku akishindwa kabisa kuzungumza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Abdullah, alitoa wito kwa Tume ya TEHAMA kuhakikisha mchakato wa tuzo unakuwa bora zaidi na unashirikisha wadau wengi zaidi.
Washiriki wa Tuzo za TEHAMA 2025 walichuana katika vipengele vya Ubunifu katika Bidhaa au Huduma za TEHAMA, Matumizi Bora ya TEHAMA, TEHAMA kwa Maendeleo ya Jamii, Kijana Aliyefanikiwa Katika TEHAMA, Wanawake Katika TEHAMA, Usalama wa TEHAMA, Mradi wa TEHAMA wa Sekta ya Umma, TEHAMA Endelevu, Tuzo za TISPA kwa Mtoa Huduma Bora ya Uunganishaji wa Mtandao na kadhalika.