DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo ndani ya Miaka 61 ya Muungano kisiasa,kiuchumi na kijamii na kuwa kielelezo cha mafanikio ya Muungano barani Afrika.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Kibada-Mwasonga Wilaya ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania.Aidha, Rais Dkt Mwinyi amesema,wananchi wa pande zote mbili wanaendelea kunufaika na matunda ya Muungano tangu kuasisiwa kwake na kufanikisha dhamira ya waasisi wake ya kuleta Uhuru,Umoja na Maendeleo ya Watanzania.
Rais Dkt.Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha Muungano kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano kwa kupitia vikao vya pamoja vya majadiliano kama ilivyofanywa na viongozi waliopita.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amefafanua kuwa,amani ya kudumu na umoja wa Watanzania ni tunu muhimu zinazopaswa kulindwa na kila Mtanzania.
Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya barabara hiyo aliyoiwekea jiwe la msingi na miradi mingine ya maendeleo ni matokeo ya kuwepo kwa amani na kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo.
Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda amani ili Taifa lipige hatua zaidi za maendeleo na kwa kuwa huu ni mwaka wa Uchaguzi amewataka kutumia haki yao kuchagua viongozi na kuhakikisha uchaguzi hauwi chanzo cha kuhatarisha amani ya nchi na kuweka mbele maslahi ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi,Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry John Silaa amesema,barabara hiyo itaifungua Wilaya ya Kigamboni kiuchumi na kuwaunganisha wananchi katika harakati za kijamii.
Barabara hiyo itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 83.8 hadi kukamilika kwake na inajengwa na Kampuni ya Estim Construction Limited.
HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI KWENYE HAFLA YA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA BARABARA YA KIBADA MWASONGA WILAYA YA KIGAMBONI DAR ES SALAAM KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 61 YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE: 25 APRILI, 2025
Mheshimiwa Abdalla Ulega;
Waziri wa Ujenzi,
Mheshimiwa Hamza Hassan Juma;
Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Albert Chalamila;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Ndugu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
Mkoa wa Dar es Salaam,
Mtendaji Mkuu wa TANROAD,
Ndugu Viongozi mbali mbali wa vyama
vya Siasa na Serikali mliopo,
Waheshimiwa Viongozi wa Dini,
Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi wa
Hafla hii na vikundi vya burdani,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ndugu Wananchi.
Mabibi na Mabwana.
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na Kutuwezesha kushiriki katika hafla hii ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kibada Mwasonga katika Wilaya hii ya Kigamboni ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania.
Napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa viongozi na Kamati ya Maandalizi kwa maandalizi mazuri na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika shughuli hii.
Aidha, nawashukuru sana viongozi wa Dini kwa dua na sala za kuiombea baraka hafla yetu hii. Vile vile, natoa shukrani kwa vikundi vya burdani kwa kuwa pamoja nasi katika kufanikisha shughuli hii muhimu ya maendeleo.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kesho tarehe 26 Aprili, 2025 nchi yetu inatimiza miaka 61 ya Muungano na kuasisiwa kwa Taifa la Tanzania.
Waasisi wa Taifa letu; Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere waliwaongoza Wananchi wa iliyokuwa Jamhuri wa Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuunda Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ni dhahiri kuwa ndani ya kipindi cha miaka 61 ya Muungano, nchi yetu imepiga hatua kubwa ya maendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii na kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kielelezo cha mafanikio ya Muungano barani Afrika.
Wananchi wa pande zote mbili za Muungano wanaendelea kunufaika na matunda ya kuasisiwa kwa Muungano wetu kwa dhamira ile ile ya waasisi wa Taifa letu ya kuleta uhuru, umoja na maendeleo ya watanzania.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani za dhati na kumpongeza Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia na kuhakikisha Muungano wa Tanzania unaendelea kuimarishwa kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano kupitia vikao vya pamoja vya majadiliano kama walivyofanya viongozi waliopita.
Aidha, nawashukuru viongozi wote wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano kwa namna wanavyoshirikiana na hivyo kuudumisha Muungano.
Hakika, ni wajibu wetu kuendeleza ushirikiano kwa faida ya kizazi cha sasa na wale watakaokuja baadae.
Ndugu Viongozi na ndugu Wananchi,
Miongoni mwa matunda makuu ya Muungano wetu ni kuendelea kuwepo kwa umoja wa Watanzania na kudumu kwa amani katika nchi yetu.
Hakika hizi ni tunu muhimu ambazo sote tuna wajibu wa kuzilinda na kuzidumisha. Umoja wa Watanzania unatoa nafasi pana kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano kunufaika na fursa mbali mbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Katika hali hiyo, hakuna mwananchi hata mmoja hapa Tanzania anayekosa faida za kuwepo kwa Muungano huu kwa namna yoyote.
Aidha, amani ya Tanzania ndio msingi mkuu wa maendeleo tunayoyapata katika sekta zote. Kwa mnasaba huo, hatua hii ya ujenzi wa miundombinu ya barabara tuliyoiwekea jiwe la msingi leo na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo, ni matokeo ya kuendelea kuwepo kwa amani nchini.
Amani tuliyonayo ndiyo inayoiwezesha Serikali kupanga na kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Hivyo, nichukue fursa hii kutoa wito kwa Watanzania wenzangu tuendelee kulinda na kudumisha amani tuliyonayo ili nchi yetu izidi kupiga hatua za maendeleo.
Kwa kuzingatia kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi sote tutumie haki yetu ya kuchagua viongozi na kuhakikisha uchaguzi huo hauwi chanzo cha kuhatarisha amani tuliyonayo.
Tuzingatie kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na hivyo tuendelee kuweka mbele maslahi ya nchi yetu kwa kudumisha amani.
Ndugu Viongozi na ndugu Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Viongozi wa Wizara na TANROAD kuhakikisha ujenzi wa barabara hii tuliyoiwekea jiwe la msingi unamalizika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba na kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, Mkandarasi ahakikishe anazingatia masharti ya mkataba na kufahamu kuwa wananchi wanasubiri kwa hamu kumalizika kwa mradi huu ili wanufaike na dhamira ya Serikali ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo yote ya Tanzania.
Ni wajibu wa wananchi kwa upande wenu kutoa ushirikiano kwa Wizara na Mkandarasi ikiwemo ulinzi wa vifaa vya ujenzi kwani vitendo kama hivyo vinaweza kuchangia kuzorotesha kasi ya kukamilisha mradi huu.
Ndugu Viongozi na ndugu Wananchi,
Nahitimisha hotuba yangu kwa kutoa shukrani zangu tena kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi katika hafla hii ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hii ya Kibada Mwasonga kwa kiwango cha lami.
Shukrani maalum nazitoa kwa Kamati ya maandalizi ya Shughuli hii na wale wote waliochangia katika kufanikisha sherehe hii.
Aidha, nawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika shughuli hii ikiwa ni kuonesha furaha yetu ya kutimiza miaka 61 ya Muungano wa Tanzania ukiwa imara zaidi na wenye mafanikio zaidi.
Nakutakieni nyote kila la kheri na maadhimisho mema ya kutimiza miaka 61 ya Muungano.
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
Ahsanteni kwa kunisikiliza
















