DAR-Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha zoezi la Urekebu wa Sheria mbalimbali nchini.

Mwandishi Mkuu wa Sheria, amesema kuwa zoezi la Urekebu wa Sheria ni moja ya majukumu ya msingi ya kikatiba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, zoezi la urekebu linahusisha kupitia sheria za nchi kwa lengo la kujumuisha marekebisho mbalimbali yaliyofanyika katika nyakati tofatui katika sheria husika.
Aidha, Bw. Njole amesema kuwa lengo kuu la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya zoezi la urekebu ni kuingizia marekebisho yaliyofanyika katika sheria mbalimbali na kuwawezesha pamoja na kuwarahisishia watumiaji wa sheria, kutumia sheria ambazo zipo na zinazokwenda na wakati.
“Kwa kutambua umuhimu wa kuwa na sheria zinazokwenda na wakati Bunge la Jamhuri lilitunga sheria mahususi inayoitwa ya Urekebu wa Sheria Sura ya 4, inayompa mamlaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia kwa Mwandishi Mkuu wa Sheria kutekeleza zoezi la urekebu wa sheria,"amesema Bw. Njole.
Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa zoezi la urekebu wa sheria linalotarajiwa kuzinduliwa hivi karibu linajumuisha jumla ya sheria kuu 446, ambapo zoezi hilo limefanyika kwa kuwatumia wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Zoezi hili la Urekebu wa sheria linahusisha jumla ya sheria Kuu za Nchi 446, pamoja na sheria ndogo takribani 30,000,"amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.

“Tunaipongeza Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiwezesha upatikanaji wa raslimali fedha na rasilimali watu ambapo kwasasa zoezi hili tunalifanya kwa wakati na kutumia wataalamu wa ndani,”amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.