DODOMA-Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya Bilioni 45 kutatua changamoto ya Maji jijini Dodoma wakati ikisubiriwa utekelezaji wa Miradi ya kuleta maji kupitia Ziwa Victoria na mradi wa Bwawa la Farkwa.

“Mbunge wenu alileta maombi kwa Mh. Rais Samia juu ya uchimbwaji wa visima virefu wakati wa mkutano wa Mh. Rais pale Mpunguzi na sisi Wizara tukapata maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kulivalia njuga suala la maji hapa Jijini Dodoma kwa kuelekeza utekelezaji wa miradi ya maji ya zaidi Tsh 45bn ambayo itasaidia sana kupunguza tatizo la mgao wa maji katika maeneo mbalimbali."

Aidha wizara ya maji kwa kushirikiana na taasisi zake (DUWASA na RUWASA) imeunda timu zinazo endelea na Utafiti wa Maji chini ya Ardhi na Uchimbaji wa visima katika maeneo ya Mzakwe, Nzuguni, Kisasa, Nkuhungu, Miganga, Zuzu, Msalato na Ihumwa.

"Nipo hapa jijini Dodoma na kesho naanza ziara maalum kukagua utekelezaji wa miradi hii ili wananchi wa Dodoma wapate maji ya uhakika,"alisema Aweso.
Akitoa taarifa yake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA), Eng. Aron Joseph amesema Mradi huu unalenga kuhudumia watu wapatao 123,095.
Kukamilika kwa mradi huu kutapelekea ongezeko la uzalishaji kutoka lita milioni 81 hadi 91 kwa siku sawa na ongezeko la 30% kutoka chanzo cha Nzuguni.