Benki Kuu yashiriki Mkutano wa Mwaka wa TAWIFA jijini Dodoma

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania imeshiriki katika mkutano wa mwaka wa Chama cha Wanawake Katika Sekta ya Fedha (TAWIFA) uliofanyika tarehe 14 Aprili 2025, jijini Dodoma. Mkutano huo uliwakutanisha wanawake kutoka taasisi mbalimbali ndani ya sekta ya fedha nchini, ukilenga kujadili masuala ya usawa wa kijinsia na ustawi wa wanawake katika maendeleo ya kiuchumi.
Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, ambaye aliipongeza TAWIFA kwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, huku akieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho kifupi.
“Wanawake nchini Tanzania wana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 35 ya Pato la Taifa linatokana na juhudi za wanawake, ambao pia wanachangia asilimia 70 ya nguvu kazi katika sekta ya kilimo, hasa katika uzalishaji wa mazao ya chakula,” alisema Dkt. Biteko.

Katika hotuba yake, Dkt. Biteko alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuwawezesha wanawake kwa kuondoa vikwazo vinavyowakabili na kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii.
Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kuwaamini na kuwapa wanawake nafasi za juu za uongozi na maamuzi, kufanya Mapitio na Tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000, kuandaa miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Ulinzi na Usalama wa Wanawake na Vijana Vyuoni uliozinduliwa mwaka 2023 na kutoa fursa nyingine mbalimbali za kifedha na kiuchumi kwa wanawake.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa TAWIFA, Bi. Nangi Massawe, ambaye alimwakilisha Naibu Gavana wa Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, alieleza kuwa TAWIFA inalenga kuwa jukwaa la kuwaleta pamoja wanawake katika sekta ya fedha kwa ajili ya kujenga sekta yenye usawa na jumuishi.

"Benki Kuu ya Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha usawa ndani ya sekta ya fedha. Tunaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha tunafikia usawa wa kijinsia kwa asilimia 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2033," alisema Bi. Massawe.
Mkutano huu ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mchango wa wanawake katika maendeleo ya kiuchumi, sambamba na kuendeleza majadiliano kuhusu masuala ya sera, uongozi, na fursa za kifedha kwa wanawake nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news