DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametangaza msamaha kwa wafungwa 4,887 ambapo wafungwa 42 wameachiliwa huru Aprili 26, 2025.
Aidha,wafungwa 4,845 wanabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 26,2025 na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,msamaha huo wa Rais Dkt.Samia ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania.
"Ni matarajio ya Serikali kuwa wafungwa hao watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.”
Miongoni mwa wafungwa wanaonufaika na msamaha huo ni wafungwa wa kunyongwa waliomaliza taratibu za kimahakama ambapo wanabadilishiwa adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha.
Pia,wafungwa waliobadilishiwa adhabu ya kifo kwa msamaha wa Rais kutoka adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha gerezani wanabadilishiwa adhabu ya kifungo cha maisha na kuwa kifungo cha miaka 30 gerezani na hawatapata punguzo.
Aidha,wengine wanaopata msamaha ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi ambao wamehukumiwa kifungo cha muda maalum au ukomo na waliokaa gerezani kwa muda wa miaka miwili na kuendelea.
Vilevile wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani au wenye watoto wanaonyonya wakiwemo wafungwa wenye ulemavu wa mwili na afya ya akili wasio na uwezo wa kufanya kazi.