Serikali yatangaza kanuni mpya za Maadili ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani 2025

DODOMA-Serikali kupitia Gazeti la Serikali Tangazo la Serikali Na. 249 la Mwaka 2025 imetangaza rasmi Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani zitakazotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 pamoja na chaguzi ndogo zitakazofuata.
Kanuni hizo, ambazo zimegawanyika katika vipengele saba vyenye vipengele vidogo vidogo, zimeweka misingi ya mwenendo unaopaswa kuzingatiwa na washiriki wote wa uchaguzi.

Zinalenga kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa haki, amani, uadilifu na kwa kuzingatia maadili ya kitaifa.

“Kanuni hizi zitatumika kuanzia siku moja baada ya tarehe ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mkuu hadi kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi,” inasomeka sehemu ya waraka huo.

Aidha, kanuni hizo zitatumika pia katika chaguzi ndogo zitakazofuata, na wahusika wake ni wagombea wa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani.

Pia,kanuni hizo zinaweka bayana kuwa ni lazima kila chama cha siasa, serikali, na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusaini na kuthibitisha kwamba watatekeleza na kuheshimu maadili hayo.

“Chama cha siasa ambacho hakitasaini Kanuni hizi za Maadili kitazuiliwa kushiriki katika uchaguzi,” inasema sehemu ya kanuni hizo.

Kwa upande wa wagombea, kabla ya uteuzi, wanatakiwa kuthibitisha kwa maandishi kuwa wataheshimu maadili hayo kwa kujaza Fomu Na.10, iliyopo katika jedwali la kwanza la kanuni.

Fomu hiyo itasainiwa mbele ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Msimamizi wa Uchaguzi au Msaidizi wa Msimamizi, na kurejeshwa pamoja na fomu ya uteuzi rasmi.
Marufuku ya Matumizi ya Simu Vituoni

Kanuni hizo zimeweka marufuku kali kuhusu matumizi ya simu za mkononi au vifaa vya mawasiliano ndani ya vituo vya kupigia kura, kuhesabia kura na kujumlishia kura.

“Ni marufuku kwa mtu yeyote kutumia simu ya mkononi au kifaa kingine cha mawasiliano ndani ya kituo cha kupigia kura,” imeeleza sehemu ya waraka huo.

Hata hivyo, kuna ruhusa maalum kwa maofisa wa uchaguzi:

“Msimamizi wa uchaguzi, msaidizi wake, msimamizi wa kituo, wasaidizi wao pamoja na mlinzi wa kituo wataruhusiwa kutumia vifaa vya mawasiliano kwa shughuli za uchaguzi tu,” inasisitiza.

Watu hao wanapaswa kuweka vifaa hivyo kwenye mtetemo au kimya ili kuepusha usumbufu.

Kanuni hizo pia zimeeleza wazi baadhi ya vitendo vinavyokatazwa vikali, ikiwa ni pamoja na:

■Kupiga kura zaidi ya mara moja katika uchaguzi mmoja.

■Kununua au kukusanya kadi za wapiga kura.

■Kuharibu kura kwa makusudi.

■Kutoa hongo, zawadi, malipo ya fedha au vifaa kwa wapiga kura au watendaji wa uchaguzi.

“Vitendo hivyo ni kinyume na maadili ya uchaguzi, na watakaobainika kuvifanya watachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria,” inaelezwa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wadau wote wa uchaguzi wakiwemo wagombea, vyama vya siasa, wanachama na wananchi – kuheshimu kanuni hizi za maadili ili uchaguzi wa mwaka 2025 ufanyike kwa amani, haki na ufanisi.

Kampeni za uelimishaji kuhusu kanuni hizo zinaendelea nchi nzima kupitia semina, warsha na vyombo vya habari, ili kuhakikisha kila mdau anafahamu wajibu wake.SOMA ZAIDI HAPA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news