DAR-Simba Sports Club (Simba SC) imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuifunga Al Masry kwa mikwaju ya penati 4-1.
Mchezo huo ulikuwa ni kisasi kwa kuwa tayari, Simba SC walikuwa wamepoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 2-0, hivyo walihitaji kupindua matokeo ili waweze kufuzu na kutinga nusu fainali.
Pia mwaka 2018 katika hatua ya awali ya michuano hii, Simba SC ilikutana na Al Masry na kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani na sare 0-0 ugenini hivyo walikuwa hawajawahi kuonja kipigo kutoka kwa Simba SC.
Ni katika mchezo uliopigwa Aprili 9,2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulienda kwenye mikwaju ya penati kufuatia ushindi wa mabao 2-0 ambao Simba iliupata kwenye dakika 90 za kawaida, matokeo ambayo yalitokea katika mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Misri.
Elie Mpanzu aliwapatia bao la kwanza dakika ya 22 kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kupokea mpira wa kurusha kutoka kwa Shomari Kapombe.
Aidha,Steve Mukwala aliwapatia bao la pili kwa kichwa dakika ya 32 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Kipindi cha pili Al Masry walitumia muda mwingi kupoteza muda huku Simba SC wakifanya mashambulizi mengi langoni kwao, lakini walikuwa imara kwenye kujilinda.
Penati za Simba zilifungwa na Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala, Kibu Denis na Shomari Kapombe.