NEW YORK-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) amesema kuwa, Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kutafsiri kwa vitendo ahadi za Beijing+30 kuelekea Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FFD4), utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Juni hadi 3 Julai 2025, Sevilla nchini Uhispania.

Alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuwawezesha wananwake na makundi mengine kiuchumi kuwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu bora kwa wasichana hasa wa maeneo ya vijijini, kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF).
Dkt. Nchemba kuwa Serikali inatoa msaada wa kisheria bure kupitia kampeni kama Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo hadi Februari 2025 ilikuwa imetoa msaada wa kisheria kwa wanawake 681,326.
“Tunatoa mafunzo ya elimu ya kifedha na ya kidijitali kwa wanawake na vijana kupitia huduma za uendelezaji wa biashara, tunatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu na kukuza bajeti jumuishi kijinsia na kuhakikisha uchambuzi wa kijinsia unajumuishwa katika upangaji na utekelezaji wa bajeti ya umma,” alisema Dkt.Nchemba.

“Tanzania inaipongeza UN Women kwa kuandaa nyaraka ya rasilimali (resource paper) inayotoa mwongozo wa kisera wa kifedha kwa mtazamo wa kijinsia. ambayo ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuhakikisha kuwa uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake unakuwa kiini cha majadiliano na matokeo ya FfD4,”aliongeza Dkt.Nchemba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Programu, Divisheni ya ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Sarah Hendriks, alisema kuwa suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi linapaswa kuwa agenda ya kudumu ya mataifa mbalimbali hususan ya kiafrika ili kujenga jamii yenye nguvu ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa mitaji, elimu, biashara na kuwawezesha kufikia masoko kwa njia ya kidigiti.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na uliwashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali duniani, wanaokutana Jijini, NewYork nchini Marekani.