MOROGORO-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepongezwa kwa uboreshwaji wa utabiri wa hali ya hewa na taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini.
Hayo yamesemwa na Mhe. Dkt. Rozalia Rwegasira, Kaimu Katibu Tawala Mkoa, sehemu ya uchumi na uzalishaji wa mkoa wa Morogoro wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Jamii Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na matukio ya Hali Mbaya ya Hewa, kwaajili ya Kupunguza Hasara na Uharibifu ,iliyofanyika mkoani Morogoro katika ukumbi wa NSSF, tarehe 15/4/2025.
“Utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuboreshwa na tahadhari za mvua kubwa na matukio ya hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa wakati na hivyo kuchangia kuokoa maisha ya watu na mali zao. Tunaishukuru na kuipongeza serikali kwa kupitia TMA kwa kazi hii njema,”amesema Dkt.Rozalia.Aidha, Dkt. Rozalia alitoa ahadi ya kushirikiana na TMA katika kufanikisha utekelezwaji wa mradi huu kwani utakuwa na faida kubwa na chanya kwa wananchi wa Tanzania.
“Katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi huu, kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tuanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na taarifa zitakazozalishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia Mradi huu, ili wadau na wananchi kwa ujumla kuweza kuchukua tahadhari kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa.”


Dkt. Chang’a alisisitiza kwamba uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu ya hali ya hewa nchini ndio chanzo kikuu cha uboreshwaji wa taarifa za hali ya hewa nchini na kuwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari zinazotolewa na TMA, na pia kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake.