ARUSHA-Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, katika siku yao ya tatu za ziara yao wametembelea Bonde la Ngorongoro na kupata nafasi ya kuona mandhari nzuri ya bonde hilo lenye kuvutia na lenye wanyama aina tofauti wakiwemo wanyama watano wakubwa duniani.
Ziara hii pia imetoa fursa kwa Wanadiplomasia kuona rasilimali za kipekee za kiasili na za kitamaduni za Tanzania ambazo Wanadiplomasia hao licha ya kukaa nchini kwa muda mrefu, wengi wao hawakuwahi kuzitembelea na kuzifahamu kwa uhalisia wake.
Ziara hiyo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ambayo imejikita katika Diplomasia ya Uchumi imelenga kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nje ya mipaka ya nchi.
Aidha, kupitia nafasi ya ushawishi waliyonayo Wanadiplomasia hao katika nchi zao, watasaidia kuwashawishi na kuhamasisha wananchi wa mataifa yao kutembelea nchini kwa wingi na kampuni za utalii za kimataifa kupata watalii wengi kuja Tanzania.
Vilevile, Wanadiplomasia wataendelea kujenga uhusiano binafsi na kubadilishana uzoefu katika kazi kutokana na umoja wanaoujenga katika ziara hii.






























