Dkt.Biteko afungua rasmi Kongamano la eLearning Africa, atoa wito

NA GODFREY NNKO

NAIBU Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dkt.Doto Biteko amefungua rasmi Kongamano la 18 la Kimataifa na Maonesho kuhusu Elimu ya Kidijitali, Mafunzo na Ukuzaji wa Ujuzi (eLearning Africa).
Kongamano hilo ambalo limeanza Mei 7,2025 limefunguliwa leo Mei 8,2025 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es likiwa ni la pili kufanyika hapa nchini tangu liasisiwe mwaka 2005.

Ethiopia ndiyo taifa la kwanza kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kubwa zaidi barani Afrika ambapo lilifanyika mwaka 2006 jijini Addis Ababa.

Mwaka 2007, Kenya walikuwa wenyeji wa kongamano hilo ambalo lilifanyikia jijini Nairobi, mwaka 2008 lilifanyika jijini Accra nchini Ghana, mwaka 2009 jijini Dakar nchini Senegal.

Aidha, Lusaka nchini Zambia lilifanyika mwaka 2010, mwaka 2011 likafanyika hapa nchini jijini Dar es Salaam, jijini Cotonou nchini Benin mwaka 2012.

Windhoek nchini Namibia mwaka 2013 walikuwa wenyeji,Kampala nchini Uganda mwaka 2014, Addis Ababa walikuwa wenyeji tena mwaka 2015.

Kwa upande wa Cairo nchini Misri walikuwa wenyeji mwaka 2016, Port Louis nchini Mauritius mwaka 2017, Kigali nchini Rwanda mwaka 2018,Abidjan nchini Ivory Coast mwaka 2019, kwa mwaka 2020 na 2021 kongamano lilifanyika kwa njia ya mtandao kutokana na changamoto ya Uviko-19.

Kigali ilikuwa mwenyeji tena wa kongamano hilo mwaka 2022,Dakar mwaka 2023, Kigali ikawa mwenyeji tena mwaka 2024.

eLearning Africa ni kongamano na maonesho ya kila mwaka ambayo huwa yanawakutanisha maelfu ya wataalamu na wadau mbalimbali kubadilishana ujuzi na maarifa kuhusu elimu ya kidijitali barani Afrika.

Katika kongamano hilo, Dkt.Biteko amewahimiza wadau wa elimu barani Afrika kuendeleza mkakati na ushirikiano utakaowezesha mageuzi ya kidigitali katika sekta ya elimu.

Pia, amesema Tanzania inaendeleza dhamira yake ya mageuzi ya kidigitali katika elimu hivyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha mafunzo kwa gharama nafuu.

Dkt.Biteko amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuongoza katika mageuzi ya kidigitali barani Afrika.

Amesema,Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inatambua kuwa mageuzi ya kidijitali ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na ushindani wa kimataifa.

Naibu Waziri Mkuu huyo amesema ili kufanikisha hilo, Serikali ya Tanzania imeandaa mifumo kadhaa ikwemo Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania 2024-2034.

Amesema kuwa,Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali na Programu ya Tanzania ya Kidijitali zinalenga kuimarisha miundombinu na huduma za kidijitali, kuhakikisha teknolojia muhimu.

Pia vifaa, muunganiko na rasilimali za eLearning kuhakikisha vinafika maeneo mbalimbali nchini.

Mbali na hayo amezitaka nchi zingine pia zitumie rasilimali zao katika kusaidia mageuzi ya kidijitali katika nchi zao.

Amewahimiza wadau wa kongamano hilo kuwa ili mageuzi ya kidijitali ya Afrika yaweze kufanikiwa, lazima kuwezeshwa kwa nguvu kazi yenye ujuzi kuanzia umri mdogo. Tanzania imefanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo mwaka 2023 na kuwa ni mfano muhimu, ikisisitiza uendelezaji wa ujuzi kuanza elimu ya msingi.

“Sera hii pia inakuza matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kukabiliana na upungufu wa walimu, kupanua upatikanaji wa elimu, na kuboresha ubora wa kujifunza.

"Mbinu hii inawaandaa wanafunzi kwa ajili ya baadaye na kuwawezesha waelimishaji kwa kuwapa zana bora za kufundishia katika nyakati za kidijitali."

Amesema,Afrika lazima iendelee kuboresha mazingira kwa kampuni za kibunifu za ndani kwa kuunda sera saidizi zinazokuza ubunifu na ujasiriamali ili kusaidia kukuza masoko ya ndani kwa teknolojia zinazoweza kuhamishika.

Dkt.Biteko pia ameyataka mataifa ya Afrika kuwezesha mataifa ya Afrika kuongeza ufanisi wa rasilimali, kupunguza ucheleweshaji na kuharakisha mageuzi ya kidijitali.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema, Tanzania imeendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu kwa kuhamasisha matumizi ya akili mnemba katika shule.

Profesa Mkenda amesema kuwa, kupitia kongamano hilo lililoanza Mei 7, 2025 litatoa fursa ya kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano katika nchi za Afrika.

Vilevile kuboresha sera na mifumo yake ya elimu ili kuendana na teknolojia, ubunifu na hususani matumizi ya Akili Unde (AI).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news