ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha maslahi ya watumishi ikiwemo nyongeza ya mishahara kuwepo kwa huduma ya afya ili kuchochea utekelezaji bora wa majukumu yao kwa dhamira ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Rais Dkt.Mwinyi amesema,Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na wafanyakazi ili kuleta maendeleo,kukuza uchumi na ustawi wa jamii katika sekta mbalimbali.

Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amekipongeza Chama cha Wafanyakazi (ZATUC) kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwezeshaji kwa maandalizi mazuri ya shughuli hiyo na kumpa heshima ya kuwa mgeni rasmi.
"Kwa hakika leo ni siku muhimu ambapo wafanyakazi na wananchi wa Zanzibar na wa Tanzania kwa jumla tunaungana na wafanyakazi wote duniani katika kuadhimisha siku hii ya muhimu.
"Mkusanyiko wetu katika siku hii unanipa faraja kubwa ya kuamini kuwa tumekuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu baina ya Serikali na wafanyakazi kupitia vyama vya wafanyakazi.

"Ninawashukuru pia kwa namna tunavyoendelea kushirikiana kupitia utatu wetu baina ya Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi jambo ambalo limetuwezesha kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili wafanyakazi hapa nchini.
"Wito wangu kwenu nyote tuendelee kuimarisha ushirikiano huu kwa faida ya pande zote ili uwe chachu ya kuleta maendeleo zaidi katika nchi yetu.
"Kupitia maadhimisho haya, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza wafanyakazi wote nchini na nawashukuru kwa juhudi zenu katika kutekeleza majukumu yenu kwenye maeneo yenu ya kazi.
"Ni dhahiri kuwa juhudi zetu za pamoja zimewezesha kuimarisha ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma mbali mbali na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya Taifa letu.
"Nawashukuru sana wafanyakazi wote nchini walioajiriwa katika Sekta rasmi na wale walioko katika sekta isiyo rasmi kwa mchango wao katika kufanikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali.
"Kwa hakika mafanikio ambayo nchi yetu inaendelea kuyapata katika sekta zote, yanatokana na juhudi zinazofanywa na wafanyakazi kwa kutimiza wajibu wao na kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo.
"Napenda niwape moyo kuwa Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa na nzuri inayofanywa na watumishi wote na hivyo tutaendelea kuchukua hatua za kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuzifanyia kazi changamoto zilizopo hatua kwa hatua.
"Serikali inatambua kazi kubwa na muhimu inayofanywa na vyama vya Wafanyakazi kama wadau muhimu wa maendeleo.
"Napenda nitumie fursa hii kuwaomba wenzetu katika vyama vya wafanyakazi na Jumuiya za Waajiri tusaidiane katika kusisitiza tunapata ufanisi wa kiutendaji miongoni mwa wanachama wenu kwa kutimiza wajibu wa kila mmoja miongoni mwenu.
"Nasema hivyo kwa kutambua kuwa bado kuna watumishi wachache wasio waadilifu ambao hawazingatii utumishi bora na wameweka mbele maslahi yao binafsi.
"Lazima watumishi wa aina hii wabadilike ili wasiwe kikwazo cha kuleta ufanisi katika kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo zaidi.
"Napenda niwaahidi kuwa, Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha watumishi wanapata haki zao na stahiki zao kwa mujibu wa sheria za utumishi na kanuni ziliopo."

"Nimefarajika kuelezwa kwamba kwa sasa vikao vitano vya wadau ambao ni Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kupitia Kamisheni ya Kazi, ZATUC na ZANEMA tayari vimefanyika na hoja 16 zimejadiliwa.
"Nimeambiwa pia Majadiliano hayo yamejumuisha Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Mfuko wa Huduma ya Afya na wadau wengine."
Amesema kuwa,tayari hoja sita zimeshapatiwa ufumbuzi, tano za ZATUC na moja ya ZANEMA na hoja saba zinaendelea na hatua za kutatuliwa.
"Ni matarajio yangu kuwa hoja zilizobaki nazo zitafanyiwa kazi na kumalizika. Ni vyema muendeleze vikao hivi vya Wadau ili kuzidi kupunguza changamoto ziliopo katika sehemu zetu za kazi na muwe mnanipa taarifa ya kila hatua za utatuzi wa changamoja hizo.
"Ni dhahiri kuwa hatua hii itaimarisha mshikamano na ushirikiano baina yetu Serikali, Wajiri na Wafanyakazi kupitia Vyama vyao. Nyote ni mashahidi wa nia na dhamira njema ya Serikali kwa wafanyakazi wake."
Rais Dkt.Mwinyi amesema,Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuboresha maslahi ya watumishi wake kwa namna mbalimbali, ikiwemo kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara (annual salary increment).
Pia, kuwa na mfuko wa huduma ya afya kwa wafanyakazi wake, pamoja na kushughulikia marekebisho ya maslahi ya watumishi baada ya kuibuka kasoro za malipo yao kufuatia kuanza kutumika ongezeko la mishahara ya wafanyakazi.
"Imani yangu ni kuwa hatua hiyo imezidi kuchochea ari ya watumishi katika kada zote kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
"Kwa mara nyingine, napenda kuwapongeza tena wafanyakazi wote nchini kwa kuadhimisha siku hii, na nawashukuru tena kwa mchango wenu katika ujenzi wa Taifa letu.
"Natumia fursa hii kutoa pongezi kwa wafanyakazi bora ambao wanatunukiwa vyeti maalum na zawadi katika sherehe hizi za Mei Mosi mwaka huu.
"Hakika, utaratibu huu unaongeza hamasa ya uwajibikaji na kuwapa ari wengine nao wajitahidi ili tuwazawadie katika miaka ijayo.
"Wito wangu kwenu wafanyakazi wote, ni kuendelea kutekeleza majukumu yenu kwa bidii, maarifa, uadilifu na uzalendo, huku mkitanguliza maslahi ya Taifa letu mbele."
Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi amewapongeza kwa kaulimbiu ya mwaka huu wa 2025 inayosema: "Wafanyakazi Tufanye Kazi kwa Bidii na Nidhamu, Tudai Haki Zetu kwa Mujibu wa Sheria na Tushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa Amani."
"Wito wangu kwa vyama vya wafanyakazi tushirikiane na Serikali na Waajiri ili kuhakikisha tunaongeza tija kwenye maeneo yetu ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.
"Kwa kuzingatia kuwa mwaka huu, nchi yetu inakabiliwa na uchaguzi mkuu, nawaomba wafanyakazi wote, viongozi, waajiri, na wananchi kwa jumla tushiriki kwa amani na kuheshimu sheria.

"Tuendelee kufanya kazi kwa bidii, na tuendelee kujenga taifa lenye haki, usawa, na maendeleo kwa maslahi na mustakabali mwema wa nchi yetu,"amefafanua kwa kina Rais Dkt.Mwinyi.