NA MARY GWERA
Mahakama Arusha
JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ameipongeza Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa kuendelea kuwa mfano katika utekelezaji wa nguzo nambari tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania inayohusu Imani kwa Wananchi na ushirikishwaji wa wadau.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akifungua Kikao cha Haki Kazi leo tarehe 15 Mei, 2025 kilichoshirikisha Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika katika ukumbi wa ‘Corridor Springs Hotel’.
Akizungumza leo tarehe 15 Mei, 2025 wakati akifungua Kikao cha Haki Kazi baina ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya ‘Corridor Springs’ jijini Arusha, Mhe. Siyani amesema jambo hili la kuwakutanisha wadau wa haki na kujadili masuala mbalimbali ni muhimu kwa mustakabali wa utendaji kazi wa Mahakama.
“Ninawapongeza Mahakama Kuu Divisheni ya kazi kwa kuendelea kuwa mfano wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama kwenye eneo hili la ushirikishwaji wa wadau, kipekee nimpongeze Mhe. Dkt Yose Mlyambina, Jaji Mfawidhi wa Divisheni hii na wenzake wamekuwa mfano bora wa ubunifu unaowezesha Mahakama na wadau wake kukutana mara kwa mara na kujengeana uwezo katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha utendaji kazi,” amesema Jaji Kiongozi.
“Hatua hii ya wadau wa Mahakama kuja pamoja kwa lengo moja ni muhimu kwa mafanikio ya taasisi yoyote na kwa Mahakama ni muhimu zaidi kwani majadiliano na uzoefu unaopatikana, unasaidia sana kuimarisha mifumo ya utoaji haki kazi nchini. Kwa hiyo, kwa dhati kabisa, ninawashukuru wadau wetu wote,” amesisitiza.
Aidha, Jaji Kiongozi ametoa wito kwa Majaji Wafawidhi na Majaji wote wa Mahakama Kuu nchini kuendelea kuimarisha ushirikiano na Wadau ili kuboresha ufanisi sambamba na kujenga Mahakama inayoshirikiana na jamii.
Ameongeza kuwa, suala la kuboresha ufanisi katika utoaji wa haki kupitia vikao kazi na mafunzo, ni jukumu endelevu kwakuwa kupitia vikao kama hivyo wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kutathmini changamoto zilizopo, kuainisha maeneo yanayohitaji maboresho na hatimaye kuandaa mikakati madhubuti itakayoimarisha kasi ya utoaji haki.
Amesema kuwa, fursa hiyo ya kukutana na wadau ni muhimu kwani inalenga kuboresha mifumo ya utoaji haki na hatimaye kuwezesha watu kupata haki kwa wakati lakini katika mazingira ya uwazi na yanayoaminika.
“Ni muhimu kukumbuka kuwa, Taifa lolote lisilo na mifumo bora ya kutoa haki, inaweza kutumbukia kwenye machafuko yasiyo ya lazima. Kwa hiyo, kwa sisi tuliopata fursa ya kuwatumikia wenzetu katika vyombo hivi, ni lazima tukumbuke wajibu wetu ambao hauwezi kukamilika kama fursa hizi muhimu za kuongeza maarifa hazitapatikana,” ameeleza.
Amesisitiza pia juu ya umuhimu wa Majaji kuendana na kasi ya mabadiliko duniani na kwamba vikao kazi kama hicho ni njia moja wapo ya kufanya hivyo.
Washiriki wa Kikao Kazi wakifuatilia kwa makini kinachoendelea katika hafla ya ufunguzi wa kikao kazi hicho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kikao Kazi kati ya Mahakama hiyo, Shirika la Kazi Duniani (ILO), Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika katika ukumbi wa ‘Corridor Springs Hotel’.
Kadhalika, Mhe. Siyani amesema kwamba, eneo la haki kazi ni muhimu kwani migogoro ya kazi sio tu inaathiri wafanyakazi na waajiri, bali maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla ambapo ameeleza kuwa, migogoro isiyoshughulikiwa kwa haraka husababisha uzalishaji kushuka, wawekezaji kupoteza imani na wakati mwingine hata kusababisha athari za kijamii kama vile migomo na hali ya kutoelewana mahala pa kazi.
Ameseisitiza kuwa, “ili kufanikisha utoaji wa haki kazi kwa wakati na kwa ufanisi, ni muhimu kwa wadau wote ikiwemo Mahakama, Ofisi ya Kamishna wa Kazi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), waajiri, wafanyakazi, OSHA, mifuko ya hifadhi ya jamii na mashirika ya kimataifa kama ILO kushirikiana kwa ukamilifu.”
Hali kadhalika amesema kuwa, Mahakama lazima iendelee kujipanga na kuboresha mifumo yake ya usikilizaji wa mashauri ya kazi, ikiwemo matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kuwezesha haki kazi kutendekea kwa wakati na gharama nafuu.
Katika neno lake la ufunguzi, Jaji Kiongozi amewasisitiza Majaji hao kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kushughulikia mashauri yote ikiwemo yale ya kazi, kuhakikisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaimarishwa ili kuboresha huduma za Mahakama, kuimarisha mafunzo ya viongozi wa Mahakama kuhusu haki kazi, sheria za kimataifa na utatuzi wa migogoro ya kazi kwa kutumia akili unde (AI).
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina amesema kuwa Kikao Kazi kimebeba Kaulimbiu isemayo ‘Uboreshaji wa Uongozi kwa Ufanisi na Tija katika Utoaji wa Haki Kazi’ na kutoa rai kwa Majaji wenzake kuwa Viongozi wa maono na kuwa Taasisi inayosimamia haki.
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ukanda wa Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kikao cha Haki Kazi baina ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika katika ukumbi wa ‘Corridor Springs Hotel’ jijini Arusha. Mkurugenzi huyo ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Shirika hilo na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Picha mbalimbali za makundi ya washiriki wa Kikao cha Haki Kazi baina ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika katika ukumbi wa ‘Corridor Springs Hotel’ jijini Arusha.(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Arusha).
Mhe. Mlyambina amesema kuwa, kikao kazi hicho kitakuwa na mada mbalimbali ambazo ni pamoja na Akili ya kihisia na udhibiti wa mafadhaiko, motisha kwa watumishi na kujenga ujasiri, uongozi na usimamizi wa mabadiliko, kanuni za maadili za uongozi na uadilifu na nyingine.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kinafanyika kwa ufadhili wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na kimehudhuriwa na Majaji Wafawidhi wote wa Mahakama Kuu nchini, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ukanda wa Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala, Kamishna wa Kazi Tanzania Bara, Bi. Suzan Mkangwa, Kamishna wa Kazi Zanzibar, Mhe. Rashid Khamis Othuman na wengine.