NA MARY GWERA
Mahakama
UJUMBE wa watumishi wa Mahakama kutoka nchini Kenya waliopo katika ziara ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho ya huduma za utoaji haki umevutiwa na kupongeza hatua kubwa ya maboresho yaliyopo ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Ikiwa ni siku ya tatu ya ziara ya ujumbe huo leo tarehe 21 Mei, 2025 wamepata fursa ya kutembelea Chumba cha Kusimamia na kuratibu Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakama ya Tanzania (Judiciary Virtual Situation Room) ambapo wamejifunza namna kinavyofanya kazi.
Akitoa taarifa kuhusu namna chumba hicho kinavyofanya kazi, Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock amesema, chumba hicho kinatoa taarifa muhimu za Mahakama ikiwemo taarifa ya idadi ya mashauri yaliyofunguliwa kwa muda husika, mashauri yaliyoamuliwa na kadhalika.
“Uwemo wa chumba hiki na mifumo mingine ya TEHAMA ni dhamira ya dhati waliyo nayo viongozi wetu kuhusu matumizi ya teknolojia, kupitia chumba hiki watumiaji wanaweza kupewa mahitaji yao kwa mujibu wa majukumu yao,” ameeleza Bw. Kalege.
Baada ya kufanya wasilisho kuhusu Chumba hivyo, wajumbe kutoka Mahakama ya Kenya walipata fursa ya kuuliza maswali pamoja na kujadiliana na watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuona jinsi gani na wao wanaweza kuanzisha chumba kama hicho katika Mahakama yao.
Ugeni kutoka Mahakama ya Kenya pamoja na wenyeji wao kutoka Mahakama ya Tanzania wakisikiliza mada iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock leo tarehe 21 Mei, 2025 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya pamoja na wenyeji wao wa Mahakama ya Tanzania wakiwa ofisini kwa Msajili Mkuu wa Mahakama walipotembelea leo tarehe 21 Mei, 2025 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Aliyeketi mbele ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya leo tarehe 21 Mei, 2025.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Aloyce Katemana akiwasilisha mada kuhusu utendaji kazi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama (Call Centre) kwa ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya leo tarehe 21 Mei, 2025.
Akiwasilisha mada kuhusu Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama (Call Centre), Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Aloyce Katemana amesema Kituo hicho kilianzishwa tarehe 01 Machi, 2022 kwa malengo ya kuimarisha imani ya wananchi na ushirikishwaji wa wadau, kuongeza uwazi juu ya huduma zinazotolewa na Mahakama, kuongeza uwajibikaji wa mfanyakazi wa Mahakama, kuwawezesha wananchi kuzifikia kwa rahisi habari za Mahakama na kwa gharama ya chini
Mhe. Katemana amesema kuwa, kituo hicho kinapokea aina mbalimbali ya mirejesho kutoka kwa wananchi na wadau kupitia namba ya bure ya 0800750247 huku akitaja mirejesho hiyo kuwa ni pamoja na maoni, malalamiko, maswali na pongezi juu ya huduma za Mahakama.
Naye Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Bi. Evetha Mboya amesema kuwa, kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kuanzisha njia nyingine ya kuwasiliana na wananchi ‘WhatsApp Chatbot’ ambayo itamuwezesha mwananchi mwenye shida yote ya Mahakama au taratibu za kisheria kuuliza swali lake na kujibiwa papo hapo kupitia ‘WhatsApp’.
Aidha, mada nyingine iliyotolewa ilihusu ‘Tathmini ya Utendaji kazi kwa Maafisa wa Mahakama kwa utoaji huduma za haki’ ambayo ilitolewa iliwasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Karol Mashauri.
Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Bi. Evetha Mboya akiwasilisha mada kuhusu utendaji kazi wa Kituo hicho mbele ya ugeni kutoka Mahakama ya Kenya uliopo katika ziara ya kujifunza kuhusu maboresho kutoka Mahakama ya Tanzania.
Ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya wakifuatilia jinsi Mtumishi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Mhe. Hamza Marishi (aliyeketi) akimuhudumia mwananchi aliyepiga simu kuomba msaada wa changamoto yake ya kisheria.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akizungumza jambo na Ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya (hawapo katika picha).
Mhe. Mashauri amesema kwamba, Miongoni mwa mageuzi ambayo Mahakama ya Tanzania imefanya ni pamoja na uanzishwaji wa Kurugenzi ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili 2014 ambapo moja ya majukumu ya kurugenzi hiyo ni kufuatilia upimaji wa utendaji wa Maafisa wa Mahakama.
Ameongeza kuwa, Mahakama imeweka viwango vya utendakazi, vya ubora na kiasi ili kupima na kutathmini utenda kazi halisi wa Maafisa wa Mahakama kulingana na mchango wao katika malengo yake.
“Kabla ya tathmini ya utendakazi ya 2015 ilikuwa ikifanywa kwa kuzingatia fomu za siri za utendaji wa kibinafsi. Mbinu hiyo ilikosa uwajibikaji na uwazi kwani mthamini hakujua vigezo vilivyotumika wala matokeo ya tathmini,” ameeleza Mhe. Mashauri na kuongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwaka 2015 Mahakama ilipitisha Mfumo wa Tathmini ya Utendaji Kazi kwa Maofisa wa Mahakama (JOPRAS) kama nyenzo muhimu katika tathmini ya utendaji kazi wa maafisa wa Mahakama.
Wasilisho lingine limetolewa kuhusu Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Square) na Msanifu Majengo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Aikamiriam Kileo ambapo ameueleza ujumbe huo kuwa, jengo hilo lina mita za mraba 63,244 na lina jumla ya sakafu tisa na mbawa (wings) tatu.
Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso akitoa mada mbele ya ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya (hawapo katika picha) waliopo nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza kutoka Mahakama ya Tanzania kuhusu maboresho mbalimbali ya utoaji haki.
Msanifu Majengo -Mahakama ya Tanzania, Bi. Aikamiriam Kileo akiwasilisha mada kuhusu Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Square) mbele ya ugeni kutoka Mahakama ya Kenya (hawapo katika picha).
Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour akiwasilisha mada kuhusu Usimamizi wa Miradi mbele ya ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya na Mahakama ya Tanzania leo tarehe 21 Mei, 2025 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Karol Mashauri akiwasilisha mada kuhusu ‘Tathmini ya Utendaji kazi kwa Maafisa wa Mahakama kwa utoaji huduma za haki’ kwa ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya waliopo nchini kujifunza kuhusu maboresho ya huduma ya utoaji haki.
Amesema usanifu wa kimahakama ‘Juditecture’ umezingatiwa katika jengo hilo ambapo amefafanua kuwa neno “Judi”- ikiashiria utawala, uwajibikaji na utoaji haki kwa wakati, "Tec"- inaashiria teknolojia ya hali ya juu ambayo imejumuishwa katika muundo wa jumla wa jengo na "Ture" -inaashiria usanifu na dhana ya kubuni ambayo imetumika kujenga jengo.
Ameongeza kuwa, jengo hilo lina jumla ya vyumba tisa vya Mahakama, kumbi ambazo zimeundwa kuchukua hadi watu 100, 60 hadi 70, huku chumba cha Mahakama kilicho katika sehemu ya kati kinaweza kuchukua zaidi ya watu 30.
Akiongezea katika wasilisho hilo, Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso amewaonesha wageni hayo miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo Mahakama imejenga kwa kutumia fedha za ndani. Miradi hiyo ni pamoja na nyumba 48 za makazi ya Majaji, ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu na miradi mingine.
Ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania na wenyeji wao kutoka Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja kwenye ofisi ya Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania walipotembelea ofisi hiyo leo tarehe 21 Mei, 2025 kwa lengo la kujifunza.
Hakimu Mkazi Mkuu na Mtaalamu Mchakata Taarifa, Mhe. Denice Mlashani akifafanua jambo kuhusu utendaji kazi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama mbele ya ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya walipotembelea Kituo hicho leo tarehe 21 Mei, 2025.(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma).
Baada ya kupata mawasilisho hayo, wajumbe hao kwa nyakati tofauti wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jitihada kubwa za maboresho ambayo imefanya na kuahidi kutekeleza waliyojifunza ili kuboresha huduma za utoaji haki nchini Kenya.
Aidha, kabla ya kupata mawasilisho hayo, Watumishi hao kutoka Mahakama ya Kenya walianza kwa kutembelea Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na kufurahishwa na uzuri wa ofisi hiyo.