NATO tutawalaumu

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS wa Urusi,Vladimir Putin ameonesha utayari wa kumaliza vita ambavyo vimedumu miaka mitatu kati yake na Ukraine huku vikiacha makovu makubwa katika nyanja zote ikiwemo kijamii na kiuchumi.
Vyanzo vya karibu na Kremlin vimenukuliwa na vyombo vya habari ikiwemo MSN vikibainisha kuwa, Putin atakuwa tayari iwapo Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (NATO) itasitisha upanuzi wake na kuondolewa kwa vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Urusi.

Hayo yanajiri katika kipindi ambacho mazungumzo ya amani yamesimama kufuatia mazungumzo ya simu kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump na Vladimir Putin.

Putin ameonekana yuko tayari kudumisha amani, lakini si kwa gharama yoyote, na anataka ahadi iliyoandikwa na kutiwa saini na wanachama wote wa NATO, wakiahidi kutotafuta kuijumuisha Moldova, Georgia au Ukraine katika umoja huo wa kijeshi.

Pia,Urusi inataka Ukraine ichukue msimamo wa kutokuwa upande wowote na kwamba baadhi ya vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Urusi viondolewe na ikiwa masharti hayo hayatatimizwa, Kremlin itaendelea na vita bila kusita.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande licha ya kuguswa na uamuzi huo wa busara kutoka Kremlin, ameona ni jambo la heri kwa NATO kutekeleza masharti hayo ili amani ya kudumu irejee. Endelea;

1.Haya masharti mazuri, hebu NATO tekeleza,
Vita hivyo si vizuri, watu vinaangamiza,
Hebu ache kusubiri, mnaweza vimaliza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

2.Kuvunjika Sovieti, ni wetu tulipongeza,
Ingelikuwa ni viti, na NATO kujimaliza,
Na badala yake eti, mwazidi kujiongeza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

3.Russia ukubwa wake, na uwezo kuongeza,
Ni wazi kwa vita vyake, hakuna kuimaliza,
Ukraine shida kwake, ndiyo inajimaliza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

4.Kama NATO mwasikia, kuamua mnaweza,
Tufurahie dunia, vita mkiimaliza,
Pale mtapoishia, tuweze kujipongeza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

5.Ukraine inakwisha, vita yaiangamiza,
Russia inaitisha, jinsi inajisogeza,
Yanapotezwa maisha, na mali kuangamiza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

6.Acheni kujieneza, Russia kujisogeza,
Vita mtavimaliza, nasi tutawapongeza,
Russia ametangaza, kumjibu mnaweza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

7.Halafu dunia yetu, ngano mmeimaliza,
Wale wakulima wetu, wanashindwa jiongeza,
Kwa hiyo chakula chetu, sasa tunabangaiza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

8.Ingekuwa huko kwenu, drone zawagaragaza,
Na halafu watu wenu, maandamano kujaza,
Mgefanya hayo yenu, ambayo mwaendeleza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

9.Sisi tunachokitaka, ni vita kuvimaliza,
Na hatunayo mashaka, mpini huo mwaweza,
Lakini mkivitaka, nchi mnaimaliza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

10.Warusi tunawataka, dunia kuendeleza,
Gesi yao twaitaka, nyumba zetu kufukiza,
Na mafuta twayataka, bei yatazipunguza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

11.Marekani tunaona, lengo vita kumaliza,
Sasa tunaowaona, vita mwaviendeleza,
Ni NATO nyie twaona, moto mnaukoleza,
Kuendelea kwa vita, NATO tutawalaumu.

12.Vita vikimalizika, Ulaya mkitangaza,
Sote tutafurahika, maisha kuendeleza,
Hatari inayonuka, nayo tutatokomeza,
Kuendelea kwa vita, NATO TUTAWALAUMU.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news