NA LWAGA MWAMBANDE
MSHAURI wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya Afya na Tiba, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,Profesa Mohamed Janabi ameshinda uchaguzi wa nafasi ya Ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.
Ni katika kikao maalum cha pili kilichoketi leo Mei 18, 2025 jijini Geneva nchini Uswisi. Profesa Janabi ameshinda kwa kura 32 kati ya kura 46.
Profesa Janabi ameshinda nafasi hiyo iliyoiachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule, Dkt.Faustine Ndugulile ambaye alifariki Novemba 27, 2024.
Aidha, Profesa Janabi anakuwa Mtanzania wa pili kushika nafasi hiyo ya juu kwenye shirika hilo kwa Ukanda wa Afrika. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kuonesha furaha ya namna yake kutokana na ushindi huo wa Profesa Janabi amesema,hakika ushindi wake ni wa Watanzania wote. Endelea;
¹Hili la Janabi letu, kwani huyu bingwa wetu,
Hapa mtumishi wetu, hadi Afrika ni yetu,
Kuchaguliwa mwenzetu, heko Serikali yetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
²Toka Muhimbili yetu, kwenda WHO shirika letu,
Hiyo hadhi kubwa kwetu, kwa Afya ya Bara letu,
Huyu mbobezi wetu, masuala Afya yetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
³Kampeni za nchi yetu, kinara Rais wetu,
Zainua watu wetu, kimataifa ni kwetu,
Tunazo hesabu zetu, hawa watalamu wetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
⁴Juzi Ndugulile wetu,alikwaa kiti chetu, akawa siyo mwenzetu, mauti ikaja kwetu,
Twaonesha tuna watu, kimataifa ni kwetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
⁵Juzi Dokta Ntuli wetu, kanyosha bendera yetu,
Naye huyu ni mwanetu, huko mwakilishi wetu,
Zote ni kampeni zetu, tena ushindani wetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
⁶Kimataifa wenzetu, washika nyadhifa zetu,
Kwa hiyo wajibu wetu, tuwaombee wenzetu,
Huko wakafanye vitu, ustawi Bara letu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
⁷Hongera Janabi wetu, kuwa Mkurugenzi wetu,
Kanda WHO Afrika yetu, ziwe njema afya zetu,
Uliyoyafanya kwetu, kazidishe kwa wenzetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
⁸Watafurahia watu, kwa kutosikika kwetu,
Maonyo mazuri kwetu, kuhusu ulaji wetu,
Afrika yako yetu, kasema na sote watu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
⁹Ingawa hubaki kwetu, tunabaki roho kwatu,
Elimu ya kwako kwetu, hiyo inabaki kuntu,
Tutajali afya zetu, kwa maisha mema yetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
¹⁰Kulakula hovyo kwetu, hizi nyamachoma zetu,
Na hivi vinywaji vyetu, athari kwa mili yetu,
Tumepunguza mwakwetu, tuko gado afya zetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
¹¹Heri kwako bingwa wetu, majukumu yako yetu,
Kwako tutapata kitu, na Waafrika wenzetu,
Zidi kuwajibika tu, akutunze Mungu wetu
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602