Rais Dkt.Samia aongeza mishahara ya wafanyakazi wa umma kwa asilimia 35.1

SINGIDA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1.
Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Mei Mosi,2025 katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Singida.

“Ninayo furaha kuwatangazia kwamba katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1.

"Nyongeza hii itakayoanza kutumika mwezi Julai mwaka huu itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 370,000 hadi shilingi 500,000.

"Ngazi nyingine za mshahara nazo zitapanda kwa kiwango kizuri jinsi bajeti inavyoturuhusu. Lakini nataka niwaambie nyongeza nzuri ipo,”amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyingine,Rais Dkt.Samia ametoa rai kwa vyama vya wafanyakazi nchini kuendelea kutoa huduma bora na kusimamia kikamilifu maslahi ya wananchama wao ili kuwaepusha na ushawishi wa kujitoa kwenye vyama vyao na kwenda kuunda vyama vingine.

“Nizungumze na wale ambao wanashawishi sehemu za kazi uundwaji wa vyama vingine vya wafanyakazi, pale kwenye vyama vya wafanyakazi hebu hili liangaliwe vizuri, Rais (TUCTA) naomba ulisimamie hilo pamoja na kamati yako.”

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),Tumaini Nyamhokya amesema, Rais Dkt.Samia amewaonesha wafanyakazi nchini moyo wa upole, kuwasilikiza na kutambua mchango wao.

Ni katika kuleta maendeleo ya ukuaji wa uchumi, hivyo wafanyakazi bado wana mpango naye kwa siku zijazo na watasimama naye pale atakapowahitaji.

Nyamhokya ameyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za TUCTA katika maadhimisho hayo ya sherehe za Mei Mosi Kitaifa mkoani Singida.

Amesema, sehemu kubwa ya madai yaliyowasilishwa kwa Rais Dkt.Samia na shirikisho hilo tayari yamefanyiwa kazi huku akiweka wazi kuwa wafanyakazi wote wanafahamu hitaji la Rais Samia mwaka huu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda amewataka wafanyakazi wa sekta zote kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za Rais Dkt.Samia katika dhana ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kuhakikisha wanatumia nishati safi ya kupikia.

Mkunda ameyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za shirikisho hilo katika maadhimisho hayo huku akieleza kuwa shirikisho hilo linatambua jitihada na hamasa kubwa za Serikali katika utunzaji wa mazingira.

Amewataka wafanyakazi wote kuhakikisha wanalibeba suala hilo na kuweka msukumo katika dhana hiyo ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Vilevile ameongeza kuwa,TUCTA inamtambua Rais Dkt.Samia kama mwanamazingira namba moja kutokana na juhudi zake za kuasisi ajenda ya nishati safi ya kupikia kitaifa na kimataifa, hivyo wanaunga mkono ajenda hiyo huku akiwataka waajiri na taasisi zote pia kuibeba ajenda hiyo muhimu ili kufanikisha lengo la matumizi ya nishati hiyo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news