Rais Dkt.Samia atangaza kifo cha Cleopa David Msuya

DAR-Aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu nstaafu, Cleopa David Msuya amefariki dunia hii leo Mei 7, 2025.
Msuya amefikwa na umauti alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kifo cha Msuya zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia Taifa.

“Kwa masikitiko makubwa natangaza kifo cha Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Msuya kilichotokea leo Mei 7, 2025 saa tatu asubuhi katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.”

"Mzee Msuya ameugua muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi ikiwemo Hospitali ya JKCI, Mzena na kule London Uingereza,” amesema Rais Dkt.Samia.

Rais Dkt.Samia ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo Mei 7 hadi 13, 2025 ambapo taarifa zaidi kuhusu msiba huo zitaendelea kutolewa na Serikali.

Msuya aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Edward Moringe Sokoine. Aliwahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu mara mbili.

Mara ya kwanza ni kuanzia tarehe 7 Novemba, 1980 hadi tarehe 24 Februari, 1983. Mara ya pili ilikuwa ni tarehe 5 Desemba, 1994 hadi tarehe 28 Novemba, 1995 huku akishika pia wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news