Sera mpya ya Mambo ya Nje kuzinduliwa mwezi huu

NA GODFREY NNKO

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania inatarajia kuzindua sera yake mpya ya Mambo ya Nje ambayo imejikita zaidi katika kulinda, kutetea maslahi ya Taifa na kukuza Diplomasia ya Uchumi.
Hayo yamesemwa leo Mei 7,2025 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo katika kikao kazi na wahariri na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Amesema, uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Mei 19,mwaka huu ikiwa ni baada ya mapitio ya Sera iliyotungwa mwaka 2001 ambapo ni zaidi ya miaka 25 iliyopita.

Balozi Kombo amebainisha kuwa, kupitia sera mpya imeanisha kwa kina namna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalinda maslahi yake upande wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni kupitia diplomasia hai.

Vilevile kujenga uchumi unaojitegemea, kutunza amani na usalama wa taifa, sambamba na kuunga mkono juhudi za kikanda na za kimataifa katika kujenga dunia bora na yenye amani.

Aidha, sera hiyo imelenga kutengeneza mazingira muhimu ambayo yataiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kikanda na kidunia na mazungumzo ya kimataifa ambapo pia Uchumi wa Buluu ni kipaumbele kikubwa.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa, baada ya hatua hiyo, Serikali inatarajia matokeo chanya katika sekta mbalimbali.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na mfumuko mkubwa wa masoko ya nje ambapo Tanzania inatarajia kuuza zaidi bidhaa nje huku akitolea mfano mazao ya korosho.

"Kwa hiyo kupitia sera hii tunatarajia masoko makubwa na ongezeko kubwa la watalii nchini."

Amesema, hiyo pia ni nafasi ya Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo kufundisha Kiswahili nje ya nchi. Pia, sera hiyo imetoa uwanda mpana wa ushirikishwaji kwa Diaspora katika masuala ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news