DODOMA-Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu (CIVE), kimewakabidhi rasmi bendera wanafunzi wanne wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika Fainali ya Mashindano ya Kimataifa ya Huawei ICT Competition, yatakayofanyika nchini China.
Hafla hiyo, iliyofanyika Mei 16, 2025, iliongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, ambaye aliwapongeza wanafunzi hao Sigfrid Michael, Paul Nkingwa, Godlove Hipolite na Felix Kuluchumila na kuwahamasisha kurejea na ushindi.
Ndaki ya CIVE imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuipeperusha bendera ya UDOM kwenye mashindano mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa, ikiendelea kuthibitisha ubora wake katika nyanja hiyo.