TABORA-Wahitimu zaidi 130 wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Milambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa Tabora wametimuliwa baada ya kuleta vurugu na kutishia kuchoma majengo ya shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amechukua uamuzi huo baada ya kupewa taarifa ya uwepo wa vurugu katika shule hiyo.
Inadaiwa wanafunzi hao walichukizwa na hatua ya uongozi wa shule hiyo kusitiza sherehe ya mahafali yao.
Akiongea na wanafunzi hao baada ya kupokea taarifa ya mienendo ya wanafunzi hao ameeleza kusikitishwa na tabia ya utovu wa nidhamu ambayo wamekuwa wakiionesha kwa walimu wao ikiwemo kutishia kuharibu miundombinu ya shule.
Chacha amesema,Serikali inajali ustawi wa shule ndiyo maana imeleta mabilioni ya fedha kwa ajili kuifanyia ukarabati mkubwa ili kuboreshwa miundombinu yake yote, ila akaonesha kukerwa na tabia zao za utovu wa nidhamu za mara kwa mara.
