DODOMA-Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana amesema,mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.9 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa.
Ameyasema hayo leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Vilevile amesema, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 209.8 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 353.1.
Ameeleza kuwa,hatua hiyo imeifanya Tanzania kuwa nafasi ya tisa duniani na kushika nafasi ya tatu barani Afrika kwa ongezeko la mapato ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya UVIKO-19.
Pia, amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), limeitaja Tanzania kuwa nchi iliyoongoza Afrika kwa mwaka 2024 kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya janga la UVIKO-19 ambapo utalii Tanzania ulikua kwa asimilia 48, Ethiopia (40%), Morocco (35%), Kenya (11%) na Tunisia (9%).
"Haya ni matokeo yaliyochagizwa na maono na kujitoa kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika filamu za Tanzania: The Royal Tour na ile ya Amazing Tanzania. "
Katika hatua nyingine amesema,idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 132.1
kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 2,141,895 mwaka 2024.
Aidha, idadi ya watalii wa ndani waliotembelea
vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 307.9 kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 3,218,352 mwaka 2024.
Waziri Chana amesema,hatua hii imewezesha idadi ya watalii kufikia 5,360,247 sawa na asilimia 107.2 ya lengo la watalii 5,000,000 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya
mwaka 2020."
