PURA yaanika mafanikio miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),Mhandisi Charles Sangweni amesema, katika kipindi cha miaka minne kuanzia Machi 2021 hadi Machi, 2025 kiwango cha gesi asilia kilichozalishwa kimefikia futi za ujazo bilioni 301.33.

Amesema,kati ya kiasi hicho futi za ujazo bilioni 142.35 zilizalishwa kutoka Kitalu cha Mnazi Bay na futi za ujazo bilioni 158.98 kutoka Kitalu cha Songo Songo.
Ameyasema hayo leo Mei 19,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kwa wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Kikao hicho kimeangazia utekelezaji wa majukumu na mafanikio yaliyopatikana katika shughuli za utafutaji,uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
"Uzalishaji huu ni wastani wa futi za ujazo bilioni 35.59 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na futi za ujazo bilioni 39.74 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo."

Mhandisi Charles Sangweni amesema,kwa kipindi cha nyuma, uzalishaji wa gesi ulikuwa wastani wa futi za ujazo bilioni 32.03 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na futi za ujazo bilioni 25.13 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo.

"Gesi asilia iliyozalishwa ilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme,matumizi ya viwandani, majumbani, taasisi na katika magari."

PURA ni nini?

PURA iliundwa kupitia kifungu namba 11, cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015. Mamlaka hiyo imeanzishwa kufuatia ongezeko la ugunduzi wa gesi asilia nchini na kubadilishwa kwa Sheria ya Petroli.
Aidha, PURA imeanzishwa ili kuleta mgawanyo mzuri wa majukumu kati ya mamlaka hiyo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) waliokuwa wakidhibiti sekta hiyo kabla ya kuanzishwa kwa PURA.

Mhandisi Sangweni amesema,PURA inatekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika kifungu namba 12 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.

Amesema, miongoni mwa majukumu ya mamlaka hiyo ni kuishauri Serikali juu ya masuala mbalimbali yanayohusu mkondo wa juu wa petroli.

Vilevile kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli na kusimamia shughuli zote za miradi ya kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).
Pia, PURA imeanzishwa ili kuendana na utaratibu mzuri wa Kimataifa wa kusimamia sekta ya petroli.

PSA

Mhandisi Charles Sangweni akizungumzia kuhusu Mkataba wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA) amesema, mikataba hiyo huwa inamtaka mwekezaji kutumia fedha zake katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia ambapo akikosa huwa anarudisha eneo kwa Serikali na kuondoka.

"Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi hapa nchini zinatekelezwa kwa kupitia utaratibu wa mikataba ya kugawana mapato ijulikanayo kama Production Sharing Agreements (PSA).

"Mikataba hii huingiwa kati ya Serikali, TPDC, na makampuni ya kimataifa ya nishati (IECs).Kwa sasa tunajumla ya mikataba 10 ambayo ipo katika hatua mbalimbali.
"Mikataba hii inaelekeza makampuni ya nje kuwekeza katika kipindi cha utafutaji ambapo pale yanapopatikana mafuta au gesi mapato hugawanywa kati ya wahusika wa mkataba kulingana na makubaliano."

Mhandisi Charles Sangweni amesema,pale mwekezaji anapopata mafuta au gesi asilia fedha zinazopatikana baada ya mauzo ya rasilimali iliyopatikana hulipa mrabaha.

Pia, hurudisha mtaji aliowekeza, hulipa kodi na tozo mbalimbali na kinachobaki hugawiwa kwa wabia wa mkataba ikiwemo Serikali na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

"Hivyo, ni muhimu kwa PURA kuhakiki kiasi cha fedha kinachowekezwa pamoja na shughuli zinazotekelezwa ili kuepuka udanganyifu unaoweza kufanywa na mwekezaji."

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema,PURA imeendelea kuhakiki na kukagua mapato na gharama za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji katika mikataba ya ugawanaji mapato kati ya Serikali na waendeshaji wa vitalu.

Lengo la kufanya hivyo ni ili kuhakikisha Serikali inapata mgawo stahiki kwenye mapato ya mafuta na gesi asilia.
"Kupitia kaguzi hizi zaidi ya shilingi bilioni 340
zimerejeshwa kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali na wawekezaji katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita."

Mhandisi Charles Sangweni amesema, fedha hizo zingeweza kutumika kama marejesho ya mtaji wa mwekezaji.

Kunadi vitalu

Wakati huo huo, Mhandisi Charles Sangweni amesema,katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali kupitia PURA imeendelea na maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Amesema,zoezi la kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kwa mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2013.

"Kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili na kwa ustawi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia kutekeleza zoezi hili muhimu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news