Waziri Mavunde awasilisha bajeti mahususi kwa miradi ya maendeleo

DODOMA-Wizara ya Madini imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia na kupitisha makadirio ya bajeti ya shilingi bilioni 224.984 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake katika mwaka wa Fedha 2025/2026.
Ombi hilo limetolewa leo Mei 2,2025 na Waziri wa Madini,Anthony Mavunde wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.

Amesema kuwa, shilingi bilioni 124,604,788,000.00 sawa na asilimia 55.38 ya bajeti yote ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 100,379,362,000.00 sawa na asilimia 44.62 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 24,268,585,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE) na shilingi bilioni 76,110,777,000.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya wizara na taasisi zilizo chini yake.

Vilevile amesema, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje katika Sekta ya Madini nchini ili kuongeza thamani ya madini hayo.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mavunde ametaja vipaumbele vya wizara mwaka ujao kuwa ni kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli.

Pia,kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa,kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati.

Aidha,wamedhamiria kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani madini,kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito,kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za madini za kina na kurasimisha

Mavunde ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuendeleza wachimbaji wadogo wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara ya madini.

Wakati huo huo, amesema wizara itaendelea na juhudi za kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuweka mazingira wezeshi yatakayowahamasisha kufanya uwekezaji.

Amesema, Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi za kifedha kutoa mikopo ya fedha na vifaa kwa wachimbaji wadogo.

Pia, kuboresha utendaji wa vituo vya mfano ili kuimarisha utoaji wa huduma na mafunzo kwa wachimbaji wadogo na kuimarisha huduma za uchorongaji kwa wachimbaji wadogo.

Waziri Mavunde amesema,wizara pia itaimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo na kuwapatia leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa za jiolojia.

Jambo lingine ni kuhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki mikutano, maonesho na makongamano mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujifunza na kutangaza shughuli zao.

Amesema,wizara inaendelea uhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki kwenye minada na maonesho ya madini.

Mbali na hayo amesema,Wizara ya Madini inaendelea kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa kipaumbele kwenye ajira zinazozalishwa katika migodi mikubwa na ya kati ya uchimbaji madini hapa nchini.

Amesema,hadi kufikia Machi 2025 kulikuwa na jumla ya ajira 19,874 ambapo ajira 19,371 sawa na asilimia 97.5 zilitolewa kwa watanzania na ajira 503 sawa na asilimia 2.5 zilikuwa za wageni.

"Ajira kwa watanzania kwenye migodi zitaendelea kuongezeka ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Madini, Sura 123 na Kanuni za Madini (Ushirikishwaji wa Watanzania) za mwaka 2018."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news