NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde anatarajiwa kuzindua Kamati ya Mawasiliano na Masoko ya Taasisi ya Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (Tanzania Mining Industry Suppliers Association-TAMISA).
TAMISA ni taasisi ya Watanzania walioungana na makundi mbalimbali ambayo yanatoa huduma kwenye sekta ya madini nchini.
Malengo yao ni pamoja na kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia ili kuwawezesha wanachama kuwa vinara wa kutoa huduma katika sekta hiyo.
Hayo yamesemwa leo Mei 14,2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Masoko ya Taasisi ya TAMISA, Dkt.Sebastian Ndege wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema, uzinduzi huo utafanyika Mei 16,2025 katika Hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam ambapo, pia waziri ataambatana na viongozi wengine waandamizi kutoka wizarani.
“Ningependa niwataarifu kuwa Mei 16,2025 tutakuwa na shughuli maalum, shughuli maalum ambayo kwanza tutakuwa tunazindua rasmi kamati yetu ambayo itakuwa inashughulika na masoko na elimu.
“Kamati hii ni maalum kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha, kuelimisha na kuwezesha wana TAMISA.
"Lakini,vilevile kutoa taarifa mbalimbali kwa wadau na Watanzania ili waweze kutambua kuwa kuna fursa mbalimbali ambazo zipo katika sekta ya madini."
Amesema, siku hiyo pia litafanyika kongamano maalum la TAMISA ambalo litaangazia kuhusu nafasi ya Watanzania katika utoaji wa huduma kwenye Sekta ya Madini.
“Sisi Watanzania tuna kila sababu ya kushiriki kwenye uchumi wa madini.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa amesema, dhumuni la kuanzisha taasisi hiyo ni ili kuwa na sauti moja.
“Hasa hasa sisi Watanzania ambao tunafanya kazi kwenye migodi, kama ambavyo mnafahamu Waziri wetu Mheshimiwa Anthony Mavunde amekuwa champion sana katika kutuhimiza sisi Watanzania tuweze kushiriki vema katika uchumi au sekta hii ya madini.
Amesema, Waziri Mavunde amekuwa akisisitiza kuwa, kuna zaidi ya shilingi trilioni 3.1 ambazo zinatumika katika manunuzi migodini.
“Sasa,sisi kama TAMISA kama sauti ya watoa huduma wengine wote ambao ni wazawa, tunajaribu kuona ni kwa namna gani ambavyo hiyo shilingi trilioni 3.1 wazawa wananufaika nayo katika kutoa huduma.”
Amesema, taasisi hiyo imedhamiria kuwajengea Watanzania uwezo ili waweze kunufaika zaidi na utoaji huduma zinazohitajika, hatua ambayo itapunguza malalamiko kuwa wageni wananufaika kupitia fursa hizo migodini.
Pia, amesema mkazo wao ni kuona ni kwa namna gani ambavyo watakuwa wanatengeneza viwanda nchini ikiwemo vya kuzalisha vipuri.
Amesema, uzalishaji wa viwanda hivyo utasaidia kutoa huduma ndani na nje ya nchi, hivyo kuwezesha Watanzania kunufaika kupitia uchumi wa madini na fursa mbalimbali zinazoambatana na sekta hiyo.
Tags
Anthony Mavunde
anzania Mining Industry Suppliers Association-TAMISA
Habari
Sekta ya Madini Tanzania
