Wizara ya Afya yatangaza ongezeko wagonjwa wa UVIKO-19

DAR-Wizara ya Afya imesema, tangu mwezi Februari hadi Aprili mwaka huu kumekuwepo na ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa 2 kati ya watu 139 waliopimwa) mwezi Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) mwezi Machi, na kisha asilimia 16.8 (wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema, kuongezeka na kupungua kwa UVIKO -19 kumekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huo mwaka 2020.

Amesema kwa kipindi hiki ongezeko hilo linaonekana zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Magembe amesema Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, na kupitia vituo vyake vya kutolea huduma imeelekeza wataalamu kuhakikisha wanaendelea kufanya utambuzi wa magonjwa hayo kwa kutumia vipimo vya maabara na kutoa matibabu stahiki kwa wagonjwa wote wanaobainika kuwa na maambukizi.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa ikiwa ni pamoja na kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kuvaa barakoa pale inapohitajika na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika mikoa ya pwani, kumekuwa na ongezeko la hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu kama Homa ya Dengue, Malaria, na magonjwa mengine ya aina hiyo, hivyo wananchi waende katika vituo vya kutolea huduma wanapoona dalili za homa, maumivu ya kichwa, macho, misuli, viungo, au vipele mwilini au dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile kikohozi, mafua, kuwashwa koo au kupumua kwa shida ili kupata vipimo na matibabu stahiki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news