DODOMA-Juni 16,2025 Kampuni ya Buckreef Gold Company Limited imesaini mkataba wa uuzaji dhahabu kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikijiunga na wazalishaji wengine wakubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza akiba ya dhahabu nchini.
Kupitia mkataba huo uliosainiwa mjini Dodoma, unaitaka Buckreef Gold kuuza angalau asilimia 20 ya uzalishaji wake wa dhahabu kwa Serikali kupitia BoT, kwa mujibu wa Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini nchini.
Hatua hii ya kimkakati inakuja wakati ambao Buckreef inapanga awamu mpya ya upanuzi itakayoongeza uzalishaji wa dhahabu kwa kiasi kikubwa na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
“Mkataba huu unaonesha jinsi tunavyoiunga mkono ajenda ya kitaifa na kujiamini kwetu katika ikolojia ya dhahabu inayokua nchini Tanzania,” alisema Bw. Isaac Bisansaba, Meneja Mkuu wa Buckreef Gold.
“Tunapojiandaa kupanua shughuli zetu, tunajivunia kushiriki katika juhudi zinazolenga kuimarisha akiba ya dhahabu ya taifa, kukuza uwezo wa usafishaji wa ndani, na kuiweka Tanzania katika nafasi bora zaidi kwenye soko la dhahabu la kimataifa.”
Mkataba huu unaiunga mkono moja kwa moja ajenda ya Serikali ya kuongeza thamani ya madini, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, na kufanikisha upatikanaji wa viwango vya kimataifa kama ithibati ya London Bullion Market Association (LBMA).
Mpango wa upanuzi wa Buckreef unajumuisha kuhamia kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi na kuongeza uwezo wa mtambo wa uchenjuaji kutoka tani 2,000 hadi 3,000 kwa siku. 

Aidha,hatua hi inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa dhahabu kufikia wastani wa wakia 62,000 kwa mwaka, na wakia 94,000 katika mwaka wa tano.
Mgodi huo una rasilimali ya tani milioni 14.4 chini ya ardhi zenye kiwango cha gramu 2.22 za dhahabu kwa tani.
Upanuzi huo pia unatarajiwa kuchochea ukuaji shirikishi katika Mkoa wa Geita, ambapo mamia ya ajira mpya zitaibuka katika sekta za uchimbaji, uhandisi, usafirishaji na uchenjuaji.
Buckreef pia imetangaza mpango wa mafunzo ya ujuzi ambapo wataalamu zaidi ya 100 wa Kitanzania watapewa mafunzo ya juu ya uchimbaji chini ya ardhi.
“Tunavyopanua shughuli zetu, ndivyo tunavyoongeza kujitolea kwetu kwa ajira za wazawa, mafunzo, na ununuzi wa ndani,” aliongeza Bisansaba.
“Tunaendelea kushirikiana kwa karibu na wasambazaji wa Kitanzania na jamii kuhakikisha ukuaji wa mgodi unaleta mafanikio kwa wote.”Buckreef Gold ni ubia kati ya Kampuni ya TRX Gold Corporation, kupitia kampuni tanzu yake ya TRX Gold Tanzania, na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Makubaliano haya ni ishara ya dhamira ya muda mrefu ya Buckreef kwa Tanzania na nafasi yake inayokua katika kuendeleza ushirikishwaji wa ndani, ongezeko la thamani, na mkakati mpana wa uboreshaji wa sekta ya madini unaosimamiwa na Serikali.
