IRINGA-Katika kuimarisha ushirikiano na wataalam wa saikolojia nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeshiriki katika Kongamano la Kitaifa la Kitaaluma la Wanasaikolojia lililowakutanisha wataalamu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kongamano hilo ambalo limechagizwa na kauli mbiu ya Saikolojia kwa Jamii yenye Afya limefanyika Juni 12 hadi 13,2025 katika Hoteli ya Gentle Hills, Iringa.
Kupitia ushiriki huo, DCEA imepata fursa ya kuwasilisha tafiti na kutoa elimu kuhusu hali ya matumizi ya dawa za kulevya nchini, pamoja na changamoto zinazohusiana na afya ya akili.
Katika kongamano hilo, DCEA ilisisitiza umuhimu wa mchango wa wanasaikolojia katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, na kutoa wito kwao kutumia ujuzi wao kitaaluma kuelimisha jamii kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo.
Sambamba na hayo, wataalam hao wamehamasishwa kujiunga na kozi fupi zinazotolewa na Colombo Plan kupitia International Society of Substance Use Professionals (ISSUP), kwa lengo la kuongeza weledi katika maeneo ya tiba, kinga na urejeshaji wa watu wenye changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na masuala ya afya ya akili.
DCEA itaendelea kushirikiana na wadau wa taaluma mbalimbali kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakuwa jumuishi, endelevu, na yenye mafanikio katika kulinda afya ya jamii ya Watanzania.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)










