Mkurugenzi wa Diaspora akutana na Mkurugenzi wa IOM jijini Dodoma

DODOMA-Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora na Fursa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Salvator Mbilinyi amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Bw. Maurizio Busatti katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Kikao hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na IOM katika utekelezaji wa mipango ya kuhamasisha na kuongeza mchango wa Watanzania waishio ughaibuni na raia wa Nchi nyingine wenye asili ya Tanzania kuchangia maendeleo ya Taifa.

Viongozi hao wamejadili mikakati ya kuendesha zoezi la utafiti wa Mtawanyiko wa Diaspora wa Tanzania duniani (Diaspora Mapping) ili kuiwezesha Serikali kupitia Wizara kukusanya, kuchambua na kuhifadhi taarifa kuhusu Diaspora ikiwa ni pamoja na kujua idadi yao, maeneo wanayoishi,ujuzi walionao, taaluma, shughuli zao za kiuchumi,kijamii na namna wanavyoweza kushiriki katika maendeleo ya nchi yao ya asili.
Katika mazungumzo hayo, IOM imewasilisha rasimu ya andiko dhana litakalowianishwa na andiko la Wizara ili kupata ufadhili kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya Uhamaji (IDF).

Ufadhili huo utasaidia kuendesha miradi ya kuchochea ushiriki wa Diaspora, ikiwemo kujifunza kutoka nchi zilizofanikiwa kuunganisha Diaspora katika maendeleo ya Taifa.
Zoezi hilo pia litaiwezesha Serikali kutumia taarifa hizo kuandaa mikakati shirikishi ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mchango wa Diaspora ili kutekeleza vipaumbele vya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la 2024, iliyozinduliwa tarehe 19 Mei 2025 jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news