NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bw.Raymond Mndolwa amesema, tume hiyo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan imerekodi mafanikio makubwa ikiwemo ongezeko la eneo la umwagiliaji.
Ni kutoka hekta 461,000 mwaka 2014/2015 hadi hekta 983,466.06 mwaka 2024/2025. Huku matarajio ni kutoka hekta 983,466.06 za sasa hadi milioni tano ifikapo mwaka 2030.
Mndolwa ameyasema hayo leo Juni 24,2025 katika kikao kazi baina ya tume hiyo na wahariri wakiwemo wamiliki mbalimbali wa vyombo vya habari nchini kinachofanyika mkoani Iringa.
Pia,amesema kuna ongezeko la utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati kutoka miradi mitatu mwaka 2021/2022 hadi 125 mwaka 2024|25.
"Na ongezeko la miradi inayosanifiwa na inayoendelea kusanifiwa ni kutoka 10 mwaka 2021/2022 hadi zaidi ya miradi 655.
"Tunachokifanya sasa hivi, mikoa yote inatekelezewa miradi, lakini mikoa ambayo ina kasi kubwa tunaiongezea spidi.Lakini,ni lazima kila mkoa kuwe na mradi wa umwagiliaji."
Mndolwa amesema kuwa, kuimarika kwa usimamizi katika matumizi ya miundombinu ya umwagiliaji kumesababisha kuongezeka kwa usajili vyama vya umwagiliaji kutoka 175 mwaka 2019/2020 hadi kufikia 909 mwaka 2024/2025.
Vilevile katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mndolwa amesema kuwa,tume inahakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga mabwawa,kuchimba visima na ujenzi wa miundombinu katika mabonde 22 ya kimkakati.
Jambo lingine ameeleza kuwa, ni kuanza matumizi ya maji kutoka Ziwa Victoria na Tanganyika.
"Kutokana na ongezeko hilo la eneo la umwagiliaji, tija katika mazao ya mpunga, mahindi, vitunguu na nyanya imeongezeka kutoka tani 1.8 hadi 2.0 kwa hekta hadi kufikia wastani wa tani 5.0 hadi 8.0 kwa hekta, tani 1.5 hadi tani 3.7 hadi 5.0, tani 13 hadi 26 na tani 5 hadi 18 kwa hekta mtawalia."
Mafanikio mengine,Bw.Mndolwa amesema ni kupatikana kwa ajira za kudumu na za muda mfupi kutokana na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.NIRC
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa mujibu wa Mndolwa iliamzishwa mwaka 2015 kwa Sheria Na.04 ya mwaka 2013.
Aidha, NIRC ni taasisi ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Kilimo ambapo ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake baada ya kutangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) Na.402 la Septemba 11,2015.
Tags
Breaking News
Habari
NIRC Tanzania
Sekta ya Kilimo Tanzania
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)


