NA GODFREY NNKO
MSAJILI wa Hazina, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu amesema kuwa, siri kubwa ya ongezeko la gawio na michango ya Serikali mwaka huu wa 2025 inachagizwa na usimamizi,malengo na mikakati mizuri inayoendelea kutekelezwa.
Gawio la mwaka 2025 limeongezeka na kufikia shilingi trilioni 1.28 kutoka mashirika ya Serikali na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, ikiwa ni ongezeko la asilimia 68 kutoka mwaka 2024.
Mchechu ameyasema hayo leo Juni 12,2025 wakati wa mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ikiwa Juni 10,2025 ofisi ya Msajili wa Hazina iliwasilisha gawio na michango hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan,Ikulu jijini Dar es Salaam.
"Siri kubwa ni usimamizi na malengo katika usimamizi. Ukiweka usimamizi mzuri, malengo mazuri na mikakati mizuri unaenda kupata hayo mapato, kama ambavyo mashamba jirani. Kwa jirani, shamba moja lina mazao mazuri, linazalisha vizuri,shamba lingine halizalishi vizuri kwa sababu tu ya usimamizi na kwa sababu ya uwekezaji."
Akielezea kuhusu pato la uwekezaji na mchango wake kwa Serikali, Msajili wa Hazina, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu amesema kuwa,linahusisha mapato yanayotokana na shughuli za uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini.
"Tunaweza kuyatazama mapato sehemu tatu, tuseme mapato sehemu mbili, lakini pesa inayoingia serikalini tunaitazama katika sehemu tatu.
"Sehemu ya kwanza ni mapato yanayotokana na kodi, sehemu ya pili ni yale mapato ambayo yanatokana na kodi ambayo yanatozwa kila mtu iwe ni sekta binafsi, iwe ni sekta ya umma wote mtatozwa kodi iwe ni mtu binafsi.
"Sehemu nyingine ni mapato yasiyo ya kikodi inawezekana ni faini za mahakamani,za polisi lakini sehemu kubwa huwa inakuwa ni kipato cha uwekezaji.Lakini, hii pia inategemea na nchi au Serikali imefanya uwekezaji mwingi kiasi gani."
Vilevile,Mchechu amesema kwa Tanzania jumla ya makampuni na taasisi 309 zina uwekezaji ambapo kati yake kampuni 56, Serikali imewekeza kwa sekta binafsi.
"Maana yake tuna asilimia 50 mpaka chini, maana yake tuna hisa chache,halafu tuna kampuni 253 ambako huko tuna hisa nyingi, kwa hiyo idadi hii inatutosha kwa sababu tumejikita katika sekta ambazo tunaona ni muhimu.
"Tuko kwenye kilimo uwekezaji wetu,tuko kwenye mabenki uwekezaji wetu, uko kwenye miundombinu uwekezaji wetu,uko kwenye mawasiliano. Lakini,hii inaisaidia Serikali siyo tu kupata hela wakati mwingine sababu za kiusalama ikitokea lolote ambalo sekta binafsi wameshindwa kuendesha, Serikali hamuanzi kujitafuta mnajua namna ya kuisaida jumuiya yenu na umma."
Mchambuzi
Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya kiuchumi,Dkt. Anthony Mveyange amesema, mashirika ya umma yanayoleta tija yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza mapato ya nchi na kupanua wigo wa mapato ya Serikali kwa ajili ya kujiletea maendeleo binafsi.
"Lakini siyo kitu kirahisi sana katika historia ya nchi za Kiafrika, mashirika ya umma ufanisi wake umekuwa changamoto, mara nyingi tumeona katika nchi nyingi mashirika ya umma yamekuwa yakilalamikiwa kama mzigo wa Serikali kwa sababu hayaleti tija.
"Hata ukiangalia katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki bado nchi nyingine hazijaweza kufanya vizuri zaidi,lakini kwa ujumla mashirika ya umma ni nguzo muhimu sana ya kusaidia kuendeleza uchumi wa nchi, ya kuendelea kusaidia uchumi wa nchi."
Amesema, hakuna uchumi wa nchi duniani ambao unaendeshwa bila ya Serikali kushika hatamu za uchumi.
"Kwa hiyo, mashirika ya umma ni sehemu pia ya hatamu za uchumi nchi."
Kuhusu mashirika mengi kujiendesha kwa hasara, Dkt.Anthony Mveyange amesema, malalamiko mengi yamekuwa yakihusu rushwa, ukiritimba na kutosimamiwa kwa ufanisi unaostahili.
"Ukiangalia kwa mfano nchi ya Uchina,labda nitoe mfano ambako mashirika ya umma yameshika sehemu kubwa ya uchumi wa nchi,suala la rushwa,ukirimba na ufanisi ambao hauna tija umepungua kwa kiasi kikubwa.
"Kwa hiyo, malalamiko mengi yamejikita hapo,kumbuka mashirika mengi ya umma kwa nchi zinazoendelea yanaendeshwa kwa pesa za Serikali, sasa kama Serikali inawekeza na mashirika hayatoi tija kwa sababu nilizozotaja changamoto ipo."
Dkt.Anthony Mveyange ameongeza kuwa, ukuaji wa mapato ya ndani unachochewa na utawala bora ambao ni nguzo muhimu ya kuyasimamia mashirika hayo yaweze kujiendesha kwa ufanisi huku akielezea pia umuhimu wa kuwekeza zaidi katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
"Kwa nchi nyingine mashirika hayo huwa yanashindanishwa na sekta binafsi ili kukidhi viwango ambavyo sekta binafsi inafanya."
Tags
Gawio Day
Gawio la Serikali
Habari
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Taasisi za Umma
Ufanisi Mashirika ya Umma
