Wapeni kisogo wanaopotosha kuhusu Uchaguzi Mkuu, Oktoba tukatiki-Dkt.Kikwete

■Ampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa usimamizi bora wa sheria na malezi kwa Mawakili wa Serikali 

■Mheshimiwa Johari asisitiza Mawakili wa Serikali ni askari wa kalamu ndani ya chama kikubwa

NA GODFREY NNKO

RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wananchi kuwapuuza wachache ambao wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kupotosha kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao.

"Wananchi, itakapofika wakati wa kupiga kura hiyo Oktoba tarehe itakayopangwa na tume, akili za kuambiwa changanya na zako. Kwa hiyo, fanyeni uamuzi wa busara ili nchi yetu iweze kupata viongozi wa kusukuma gurudumu la maendeleo mbele."
Ameyasema hayo leo Juni 21,2025 katika Kongamano la Kitaifa la Sheria ambalo linafanyikia ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo ambalo limeratibiwa na Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), limechagizwa na kauli mbiu ya Demokrasia kwa Vitendo:Sheria,Uwajibikaji na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Dkt.Kikwete amesema kuwa, Serikali kupitia Tume Huru ya Uchaguzi imeshafanya marekebisho makubwa kwenye mifumo ya uchaguzi.

Huku akitolea mfano kuwa, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 imewaondoa Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia Uchaguzi badala yake tume itateua yenyewe, pia imeondoa changamoto ya wagombea kupita bila kupingwa na mambo mengine.

"Kwa hiyo, hayo ni mabadiliko ambayo yana manufaa makubwa katika Demokrasia na uchaguzi."

Amesema, mbali na elimu pia Mawakili wa Serikali kupitia kongamano hili watasaidia wananchi kufahamu kuhusu haki ya kupiga kura na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi kama njia ya kushiriki katika utawala wa nchi.

"Katika kipindi hiki ambacho imebaki miezi michache kabla ya uchaguzi wa Rais,wabunge na madiwani, kukutana kwenu kufanya kongamano hili ni muhimu sana. Tanzania ni nchi yenye historia ndefu ya safari ya kidemokrasia tangu uhuru hadi Muungano."

Dkt.Kikwete ameeleza kuwa, mjadala wa leo una umuhimu wa kipekee kwa Taifa ikizingatiwa mada zitaangazia kuhusu maboresho ya sheria za uchaguzi, amani, vyombo vya dola na mengineyo kuelekea Uchaguzi Mkuu.

"Chama hiki nimeambiwa kina wanachama takribani 4,000 ili si jeshi dogo, kama taratibu za kijeshi hili ni zaidi ya brigedi. Kwa hiyo ninafurahi licha ya uchanga wenu mmefanya mambo makubwa."

Amesema, huko mbeleni anaamini chama hicho kitafaya mambo makubwa zaidi kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia, amempongeza Mwanasheria Mkuu wa wa Serikali,Mheshimiwa Johari Hamza kwa kazi nzuri anayoifanya kupitia ofisi yake na malezi bora anayotoa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali.

PBA

Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, wakili Bavoo Junus amesema, wameona ni vema kuandaa kongamano hilo hili, ili pamoja na mambo mengine Watanzania waweze kupata uelewa mpana kuhusu masuala ya Uchaguzi Mkuu.

Wakili Junus amesema,moja kati ya malengo ya kuanzishwa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) ni kuwaunganisha Mawakili wa Serikali wanaotoka katika maeneo mbalimbali nchini.

Lengo ni ili kuwaleta pamoja kuweza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sheria, lakini pia lengo lingine la msingi la kuanzishwa kwa chama ni kukifanya chama kiwe jukwaa la kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi.

"Kwa sababu Serikali inawajibika kwa wananchi, kwa maana hiyo sisi ni mawakili wa wananchi."

Ameongeza kuwa, Chama cha Mawakili wa Serikali kina jukumu la kutoa elimu katika masuala mbalimbali ya kisheria hasa katika mambo yanayogusa maslahi mapana ya Taifa.

Pia, wakili Junus amesema, katika kutekeleza jukumu la kutoa elimu kwa umma, na kwa kuzingatia Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania kimeandaa kongamano hilo ambalo lengo lake kubwa ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria mbalimbali zinazohusu uchaguzi huo.

Dar

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewahakikishia wananchi kuwa, uchaguzi mkuu ujao utafanyika kwa amani na utulivu.

Mpogolo licha ya kuwahimiza wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano kwa sasa,kabla na baada ya uchaguzi,pia amewataka wananchi kuwapa kisogo watu wenye kupigania maslahi yao ili kujinufaisha.

Johari

Naye mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Johari Hamza amesema kuwa, mawakili wa Serikali ni nguzo muhimu kwa ustawi wa jamii na Taifa.

"Sisi Mawakili wa Serikali ni askari wa kalamu ndani ya chama kikubwa.Hili ni kongamano la kwanza tangu tulipoanzisha chama hiki."

Amesema,elimu wanatoa kwa wananchi hasa katika kipindi ambacho kuna uhitaji mkubwa kwa wananchi ili waweze kupata uelewa mpana na waweze kufanya maamuzi sahihi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, dhamira ya kongamano ni kuendelea kuwaelimisha na kuwajengea uelewa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na sheria.

Vilevile, Mheshimiwa Johari amesema, mabadiliko ya sheria mbalimbali za Uchaguzi yaliyofanyika mwaka 2024 yalitokana na maombi ya wadau mbalimbali, wakiwemo wanasiasa na vyama vya siasa.

Amesema kuwa,baada ya kupokea maombi hayo, Serikali ilikusanya maoni kuhusu mabadiliko hayo, ikiwemo kubadilisha Sheria ya Uchaguzi na kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa, na hatua hizo sasa zimekamilika.

Mheshimiwa Johari ameongeza kuwa, kupitia Kongamano la Kitaifa la Sheria, wananchi wanapata fursa ya kufahamu marekebisho muhimu yaliyofanyika.

"Vyama vya siasa vyote vilishiriki katika mchakato mzima wa mabadiliko ya sheria za uchaguzi, zikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa. Nashangaa kuona wapo wanaodai hakuna reforms zilizofanyika kuhusu masuala ya uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi."

Mheshimwa Johari amemshukuru Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo muhimu ambalo linaweka msingi wa uelewa wa sheria kuelekea uchaguzi.

Sagini

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Jumanne Sagini (Mb) kwa niaba ya Waziri Dkt.Damas Ndumbaro amesema,kongamano hili jumuishi ambalo linaangazia masuala ya Uchaguzi ujao linawapa uwanda mpana wananchi kuweza kuelewa kuhusu Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

Amesema, kupitia elimu inayotolewa itawapa nafasi wananchi kutambua namna ambavyo Serikali imejipanga kusimamia na kuendesha uchaguzi huru na wa haki nchini.

Mbali na kuwapongeza Mawakili wa Serikali kwa kuja na ubunifu huo,pia amewahimiza wadau wengine ikiwemo Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuja na utaratibu huo wa kutoa elimu kwa umma.

Amesema, uwepo wa kongamano hili ni kielelezo tosha kuwa, Tanzania ina ukomavu wa kidemokrasia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news