■Wananchi wapongeza uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kupitisha majina mapya
■Waangusha vitoweo vya kutosha wakisema miaka miaka 15 haikuwa ya furaha kwao
TANGA-Furaha, nderemo na vifijo vimetawala katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Bumbuli baada ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza majina ya watia nia waliopitishwa kuendelea na mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya ubunge wa 2025 bila jina la Mbunge aliyekuwepo, January Makamba, kurejeshwa.
.jpeg)
Wananchi wa Bumbuli, wakiwemo vijana, wazee na wanawake, walijitokeza kwa wingi kusherehekea kile walichokiita "ukurasa mpya wa demokrasia ndani ya CCM na jimbo lao."
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameeleza kuwa, uamuzi huo wa Kamati Kuu ni ushahidi wa kusikiliza sauti ya wananchi waliotamani mabadiliko ya kweli baada ya miaka 15 ya uongozi wa January Makamba.
"Hii ni siku ya kihistoria kwetu. Tumekuwa tukililia mabadiliko kwa muda mrefu, sasa chama kimetusikiliza. Tunashukuru Kamati Kuu kwa kutupa nafasi ya kuandika upya historia ya Bumbuli,"amesema Bi. Amina Rashid, mkazi wa Soni.
Wadau mbalimbali wa siasa na maendeleo jimboni humo wameeleza matumaini yao kuwa hatua hii itafungua milango kwa viongozi wapya wenye dira na ari ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
Kwa sasa, macho na masikio ya wakazi wa Bumbuli yameelekezwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, huku wengi wakiahidi kushiriki kikamilifu kuhakikisha wanapata kiongozi atakayekuwa sauti ya watu bungeni.
Tags
Habari