Dar yawaleta pamoja viongozi waandamizi wa SADC

NA GODFREY NNKO 

MKUTANO wa 27 wa Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO) umeanza leo katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ambao umetanguliwa na Kikao cha Kamati ya Kudumu cha Makatibu Wakuu umefunguliwa leo Julai 21,2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Dkt. Samwel William Shelukindo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Katika hotuba yake, Balozi Shelukindo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukuza amani na usalama katika kanda hiyo.

"Mkutano wetu, ambao ni utangulizi wa Kamati ya Mawaziri ya MCO, unatupa fursa muhimu ya kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyoidhinishwa na mikutano ya viongozi, mabaraza na mikutano yetu ya awali, ikiwa ni pamoja na Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri ya MCO uliofanyika Lusaka mwezi Julai,mwaka jana.

"Tutazingatia pia kwa undani taarifa kutoka Kamati ya Siasa na Kidiplomasia kati ya nchi, Kamati ya Ulinzi na Usalama kati ya nchi, Kamati Ndogo ya Usalama wa Umma.
"Vilevile Kamati Ndogo ya Kupambana na Rushwa,Kamati Ndogo ya Magereza/Urekebu, SARPCO na Usalama wa Taifa."

Balozi Dkt.Shelukindo amesema,mkutano huu unalenga kujadili maendeleo ya utekelezaji wa maamuzi ya SADC, kutathmini taarifa kutoka kamati mbalimbali na kushughulikia changamoto za kikanda, ikiwa ni pamoja na vitisho vya usalama katika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Pia, Dkt.Shelukindo amewakumbuka viongozi wa zamani waliotangulia mbele ya haki, akiwemo Rais wa zamani wa Zambia Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu na Makamu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mheshimiwa David Mabuza, na kuongoza dakika moja ya ukimya kwa ajili ya kuwaenzi marehemu hao.
"Kabla ya kuendelea, naomba kutoa salamu zetu za rambirambi kwa Serikali na watu wa Jamhuri ya Zambia kufuatia kifo cha Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Zambia, aliyefariki mwezi uliopita.

"Jumuiya nzima ya SADC itamkumbuka marehemu Rais Lungu kama kiongozi aliyeitumikia nchi yake kwa bidii na aliyechangia pakubwa katika malengo ya mshikamano na umoja wa kikanda.

"Tunatoa pia pole zetu za dhati kwa Serikali na watu wa Jamhuri ya Afrika Kusini kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais wa zamani Mheshimiwa David Mabuza, ambaye uongozi wake ulionesha dhamira ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii.Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia zao na wote wanaoomboleza msiba huu mzito."
"Tunatoa pia heshima kwa askari wetu mashujaa waliotoa maisha yao wakiwa kazini chini ya Operesheni ya SADC nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC)."

Mkutano huu unatarajiwa kuwa jukwaa la majadiliano kuhusu masuala ya amani na usalama wa kikanda na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news