ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, amesema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) imeonesha mafanikio makubwa na ya kupigiwa mfano katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la Shirikisho la Walimu Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Utaani, Wete Pemba, Mheshimiwa Hemed alisema hatua zilizochukuliwa na wizara hiyo zimeimarisha sekta ya elimu Zanzibar na kuchangia moja kwa moja kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi.
“Katika kipindi hiki, skuli 36 za ghorofa kwa ngazi ya msingi na sekondari zimejengwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar. Skuli hizo ni za kisasa na zina vifaa muhimu kama maabara za sayansi, maktaba, vyumba vya kompyuta na vyoo bora,” alisema Mhe. Hemed.
Aidha, zaidi ya vitabu milioni 3 vya kufundishia na kujifunzia vimesambazwa katika skuli zote, hatua ambayo imesaidia kuboresha mazingira ya ujifunzaji.
Serikali pia imeongeza ajira kwa walimu na kufikia walimu 3,531 ifikapo mwaka 2025, sambamba na kuongezeka kwa bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu hadi shilingi bilioni 33.4.
Mhe. Hemed alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane pia imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi hadi kufikia 3,409, huku majengo 21 ya dakhalia yakikamilika na mengine 14 yakiendelea kujengwa Unguja na Pemba.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara, bandari, viwanja vya ndege, huduma za afya, elimu na uchumi wa buluu kwa lengo la kuinua maisha ya wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa, amesema Shirikisho la Walimu linaishukuru Serikali kwa kuipa hadhi sekta ya elimu na kuwajali walimu, hatua iliyoleta hamasa na morali kazini.
Akisoma risala ya Shirikisho la Walimu, Mwalimu Khamis Othman alisema kongamano hilo limelenga kutoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi zao za kuimarisha elimu nchini.
