TABORA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limemfukuza kazi askari wake Koplo Gebasa G.8265 ambaye alikuwa kazi kituo kidogo cha Polisi Kata ya Sungwizi Tarafa ya Simbo Wilaya ya Igunga kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishina Msaidizi, Richard Abwao amethibitisha kufukuzwa kwa askari huyo ambapo uamuzi wa kumfukuza kazi askari huyo umekuja baada ya kufanya uchunguzi wa kina kutokana na tuhuma iliyokuwa ikimkabili ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili Februali 22, 2025.
Amesema, siku ya tukio majira ya saa 3:30, usiku katika uwanja wa mpira jirani na Shule ya Sekondari Nkinga, askari huyo alituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16 ambaye jina lake limehifadhiwa.
Kamanda huyo amesema,baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hiyo, walimkamata askari huyo, kisha kumuweka mahabusu ambapo uchunguzi ulifanyika kwa kina na kubaini askari huyo alishindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi, badala yake alijihusisha na kitendo hicho.
“Mimi kama kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, nimefanya hivyo ikiwa ni moja ya majukumu yangu ya kusimamia nidhamu ya askari wote.Napenda kutoa onyo kali kwa askari yoyote atakaye bainika kufanya upuuzi kama huo hatutasita kumfukuza kazi,huku akitoa onyo pia kwa baadhi ya wananchi wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwa kuwa watakaobainika nao watakamatwa na kufikishwa mahakamani."
.jpeg)