BoT yashiriki Mkutano wa 47 wa Mwaka wa Chama cha Mabenki Kuu ya Afrika (AACB) nchini Cameroon

Mkutano huo uliendeshwa chini ya kaulimbiu “Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Utulivu wa Uchumi Mkuu: Jukumu la Benki Kuu” na kuongozwa na Mwenyekiti wa kikao, Gavana wa Benki Kuu ya Mauritius, Dkt. Priscilla Muthoora Thakoor.

Mkutano huo wa ngazi ya juu uliofanyika tarehe 28 Novemba 2025, ulihitimisha mfululizo wa vikao vya kiufundi pamoja na Kongamano la Magavana, na kuwakutanisha viongozi wa benki kuu, watunga sera, na washirika wa kimataifa lengo likiwa kuendeleza ajenda ya ushirikiano wa kifedha barani Afrika.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Gavana wa Benki ya Mataifa ya Afrika ya Kati (BEAC), Yvon Sana Bangui, alibainisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa changamoto halisi inayozikabili mamlaka za fedha.

Alisisitiza kuwa athari zake zinaonekana moja kwa moja katika uchumi, mifumo ya fedha, na uthabiti wa mataifa, hivyo benki kuu zina wajibu wa kujumuisha hatari hizo katika sera, mifumo ya uchumi mkuu, na vyombo vya kulinda utulivu wa kifedha.
Mada kuu ya mkutano ilikuwa kupitia maendeleo yaliyopatikana chini ya Mpango wa Ushirikiano wa Kifedha wa Afrika (AMCP), ambao ni msingi muhimu unaoongoza safari ya bara hilo kuelekea muunganiko na utangamano wa kifedha.

Aidha, Magavana walijadili uharakishaji wa kuanzishwa kwa Taasisi ya Fedha ya Afrika, wakaidhinisha programu ya kazi ya mwaka 2026–2028 ya Jumuiya ya Wasimamizi wa Benki za Afrika, na kujadili mbinu za kuimarisha ushirikiano wa mifumo ya malipo kwa kutumia miundombinu ya kitaifa na kikanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news