ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo amewaongoza viongozi na wananchi mbalimbali katika mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa mstaafu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, marehemu Abdalla Mwinyi Khamis ambaye alifariki dunia jana akiwa hospitalini.

Marehemu Abdallah Mwinyi alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lumumba.
Mapema leo Rais Dkt. Mwinyi alijumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Jeneza iliyosaliwa katika Msikiti wa Jamiu Zinjibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, kabla ya kuelekea kwenye maziko.
Marehemu Abdalla Mwinyi Khamis ambaye alijulikana kwa huduma yake ya uongozi, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na Meneja wa Uwanja wa Amani, Mkurugenzi wa Idara ya Television ya Zanzibar (TVZ), Mshauri wa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Maziko ya marehemu Abdalla Mwinyi yamefanyika leo kijijini kwao Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi.







