ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepokea mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za Mashindano ya Africa Federation Sports Festival, yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar hivi karibuni.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwashirikisha wanamichezo zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali duniani, ambao watawasili Zanzibar kushiriki mashindano hayo ya kwanza kufanyika hapa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amezungumza na Viongozi Wakuu wa Taasisi ya Africa Federation, akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Africa Federation, Fadhal Kassam ambaye ameambatana na Katibu wa Islamic Jamaat Zanzibar, Akbar Hassanali leo Disemba 12,2025 waliofika Ikulu,Zanzibar.
Mashindano hayo yatashirikisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, volleyball, table tennis na mbio za baiskeli, na yanatarajiwa kuanza kuanzia tarehe 24 hadi 28 Disemba 2025 katika Viwanja vya Maisara Sports Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.
