Rais Dkt.Mwinyi avihimiza vyuo vikuu Zanzibar kuimarisha tafiti zitakazotatua changamoto za jamii

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezihimiza Vyuo Vikuu vya Zanzibar kuongeza kasi ya kufanya tafiti zenye tija zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa rai hiyo leo Disemba 13,2025 alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al Sumait, yaliyofanyika Chukwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema, tafiti nyingi zimekuwa zikifanyika katika vyuo vikuu, lakini hazitumiki wala kusambazwa kwa jamii, hali inayozifanya kushindwa kuchangia kikamilifu katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi. 

Amesisitiza kuwa,tafiti zisipotumika hushusha hadhi ya vyuo vikuu na kupunguza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al Sumait katika kuandaa wataalamu wa fani mbalimbali, na kuahidi kuendelea kukiunga mkono ili kiendelee kutekeleza majukumu yake ya kitaaluma kwa ufanisi.

Vilevile, ameipongeza sekta binafsi kwa mchango wake katika kukuza elimu nchini, pamoja na Taasisi ya Direct Aid ya Korea kwa mchango mkubwa unaoendelea kutoa kwa Chuo hicho na kwa maendeleo ya sekta ya elimu kwa ujumla.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuanzisha kozi mpya ikiwemo Shahada ya Uzamili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) pamoja na kozi za muda mfupi kwa watumishi wa umma.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 679 wametunukiwa Shahada ya Kwanza, Shahada ya Uzamili, Stashahada na Astashahada, ambapo asilimia 64.5 ni wanawake na asilimia 35.5 ni wanaume.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amewataka wahitimu hao kuwa chachu ya mabadiliko chanya, kuishi kwa maadili na nidhamu, na kuchangia kikamilifu maendeleo ya Taifa na jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al Sumait, ambaye ni Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume, amesema elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya mwanadamu na kuahidi kuwa Chuo hicho kitaendelea kutoa mchango wake katika kukuza elimu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news