DODOMA-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kikao cha Tatu cha Kamati Maalum ya Usimamizi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu Mageuzi ya Taasisi za Umoja wa Afrika (AU) kilichofanyika kwa njia ya mtandao Januari 29, 2026.

Kikao hicho ambacho kimejadili na kupokea michango mbalimbali ya wajumbe kuhusu kuboresha Taasisi za Umoja wa Afrika kiliongozwa na Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. William Ruto.
Pamoja na mambo mengine, mageuzi katika Umoja wa Afrika yanalenga katika kuimarisha utawala bora, amani na usalama Barani Afrika, kuimarisha ufanisi wa kitaasisi, kuhakikisha ufadhili endelevu, kurahisisha ufanyaji maamuzi na kuiwezesha AU kufanikisha na kutekeleza matarajio ya Agenda ya Afrika ya mwaka 2063.




